Baada ya Gesi ya Mtwara, Hifadhi Kubwa Zaidi ya Gesi ya HELIUM Yagunduliwa Tanzania




GESI ya helium ya takribani futi za ujazo bilioni 54 inayoelezwa kuwa adimu duniani, imegundulika nchini Tanzania na kuiweka nchi kuwa miongoni mwa mataifa machache yenye madini mengi na muhimu.


Wagunduzi wa gesi hiyo ni watafiti kutoka vyuo vikuu viwili nchini Uingereza vya Oxford na Durham kwa kushirikiana na wataalamu wa madini kutoka nchini Norway.


Watafiti hao wamegundua hifadhi kubwa zaidi duniani ya gesi hiyo ya barafu, kama inavyofahamika katika eneo la Bonde la Ufa nchini.


Taarifa za waandishi wa habari nchini Japan, zimeeleza kuwa watafiti hao wamesema kuwa uhaba wa gesi hiyo duniani ulikuwa umesababisha taharuki haswa kwa madaktari, ambao wanatumia gesi hiyo adimu kuendesha mashine za utabibu zijulikanazo kama ‘MRI scanners’.


Pia hutumia katika mitambo ya kinyuklia na katika sekta nyingine nyingi za kiteknolojia.


Wiki iliyopita, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo wakati akijibu swali bungeni mjini Dodoma alisema madini yanayotumika kwa ajili ya mitambo ya Apollo na pia vifaa vya matibabu kama MRI na NMR, yamegundulika kuwepo nchini Tanzania.


Hata hivyo, hakufafanua zaidi kiasi cha madini hayo na namna nchi itakavyonufaika na ugunduzi huo. Hata alipotafutwa jana, simu yake ya mkononi ilipokewa na msaidizi wake na kueleza kuwa waziri yuko kikaoni. Madini aina ya helium yanatumika kwa ajili ya mitambo na pia kwenye vifaa vya matibabu kama MRI na NMR.


Kabla ugunduzi huo, watafiti walikuwa wamebashiri ukosefu wa gesi hiyo ifikapo mwaka wa 2035.


Mnamo mwaka 2010, mwanasayansi ambaye alikuwa mshindi ya Tuzo la Nobel, Robert Richardson alitabiri kumalizika kwa gesi hiyo katika kipindi kifupi. Ukosefu huo ulikuwa umesababisha wataalamu, kuhimiza kutungwa kwa sheria itakayopunguza matumizi yake katika bidhaa zisizo za dharura.


Mtaalamu kutoka Chuo Kikuu cha Oxford, Chris Ballentine alisema gesi hiyo iliyopatikana nchini inaweza kujaza silinda za gesi milioni 1.2 za mashine za MRI.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527