WAZIRI MKUU MAJALIWA ACHEKELEA TUZO ZA LULU NA RICHIE,ANGALIA PICHA HAPA
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imefarijaka kwa ushindi wa wasanii wa filamu nchini walioshinda tuzo za filamu Afrika za mwaka 2016(African Magic Viewers Choice Award) ziliyofanyika jijini Lagos nchini Nigeria mwishoni wa wiki iliyopita.


Waziri Mkuu Majaliwa, amesema hayo leo katika ukumbi wa mikutano ulipo katika Ofisi yake Jijini Dares Salaam, alipokutana na washindi wa tuzo za filamu Afrika za mwaka 2016 (AMVCA) ambao ni Elizabeth Michael ‘Lulu’ aliyeshinda tuzo ya Filamu Bora ya Afrika Mashariki na Single Mtambalike ‘Richie’ aliyeshinda tuzo ya Filamu Bora ya Kiswahili pamoja Naibu Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo, Mhe. Annastazia Wambura,Katibu Mkuu wa wizara Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo, Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Bi Joyce Fisso na wasanii wa filamu.


“Serikali imefarijika sana kwa nyie kwenda Nigeria na kushinda na mmetumia lugha ya Kiswahili, lazima tutumie nafasi hii kuwatangaza pia mmuendelee na fani hii ili kuvutia wengi zaidi” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.


Aidha, Waziri Mkuu amewapongeza wasanii hao na kusema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wasanii wakati wowote na amewataka kujipanga vizuri kutumia vyama vyao vya sanaa na kusisitiza kuwa Mhe. Rais John Pombe Magufuli ametoa matamko kadhaa kuhusu sanaa na wasanii na ameendelea kushughulikia malalamiko yao ikiwemo suala la COSOTA, na kusema kuwa baada ya taratibu zote kukamilika suala hilo litasimamiwa na Wizara inayohusika na kazi za Sanaa.


Waziri Mkuu Majaliwa, pia amewataka watanzania kuacha tabia ya kutojiamini na kujidharau, na kuwataka watu waige mfano kwa wasanii hao, na kuwashauri wasanii wote kwa ujumla kutumia vyombo vya habari kujiimarisha na kujitangaza.


Kwa upande wao, wasanii waliopata tuzo hizo kwa filamu ya “mapenzi ya Mungu” ya Elizabeth Michael na filamu ya “Kitendawili” ya Single Mtambalike, wameishukuru Serikali kwa kuwathamini na kuonesha ushirikiano katika kazi zao za sanaa, na wameahidi kuendelea kutengeneza kazi nzuri za sanaa ili ziweze kuitangaza Tanzania kimataifa.


Naye, Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania(TAFF) Saimon Mwakifamba ameishukuru Serikali kwa jitihada mbalimbali inazofanya katika kusaidia tasnia ya sanaa kwa ujumla na ameahidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuendeleza tasnia hiyo kimataifa.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea Tuzo kutoka kwa Msanii wa filamu Elizabeth Michael ambayo msanii huyo alishinda nchini Nigearia. Tukio hilo lilifanyika Ofisini kwa Waziri Mkuu jijini Dar es salaam Machi 11, 2016.

Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa akipokea tuzo kutoka kwa msanii wa filamu, Single Mtambalike ambayo msanii huyo alishinda nchini Nigeria. Tukio hilo lilifanyika Ofisini kwa Waziri Mkuu jijini Dar es salaam Machi 11, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527