RAIS MTEULE WA ZANZIBAR DK SHEIN KUAPISHWA ALHAMIS WIKI HII,BAADA YA KUAPISHWA ATAUNDA SERIKALI YAKE



Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema kuwa sherehe za kuapishwa kwa Rais mteule wa Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein zitafanyika siku ya Alhamisi Machi 24 katika uwanja wa Amaan, na maandalizi yote yamekamilika katika shughuli hiyo inayotarajiwa kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Rais John Pombe Magufuli pamoja na viongozi wengine wa kitaifa.


Siku hiyo imetangazwa kuwa ni ya mapumziko kwa upande wa Zanzibar ili kuwapa fursa wananchi kuhudhuria kwa wingi katika hafla hiyo.


Tamko hilo limetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Bwana Mohamed Aboud katika mahojiano maalum kuhusiana na maandalizi ya kuapishwa kwa Rais mteule wa Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein ikiwa ni siku chache tangu kutangazwa kuwa mshindi wa nafasi hiyo katika uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi 20 mwaka huu.



Waziri Aboud amesema mbali na Viongozi wa kitaifa, Mawaziri wa Serikali zote mbili, Wabunge, Viongozi wa vyama vya upinzani, Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa Tanzania, viongozi wa dini na asasi za kiraia pia wamealikwa katika sherehe hiyo itakayofanyika kuanza asubuhi na kumalizika saa saba za mchana.


Akizungumzia kitendawili cha hatma ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Waziri Aboud amesema kuwa mara baada ya kuapishwa kwa Rais, ataunda Serikali yake kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar.



Aidha, Waziri Aboud amewataka wananchi wa Zanzibar hasa wafuasi wa Chama cha Mapinduzi kuendelea kusherehekea ushindi wao bila ya kumbughudhi mtu yoyote na kuendelea kudumisha hali ya amani na utulivu visiwani hapa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527