WANAOISHI NA VIRUSI VYA UKIMWI WATANGAZIWA NEEMA


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikata utepe kuashiria uzinduzi wa kampeni ya kitaifa ya kupima Virusi vya UKIMWI (VVU) na kuanza kutumia dawa mapema inayojulikana kama Furaha Yangu iliyofanyika katika uwanja wa Jamhuri, Jijini Dodoma.
***
Watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (VVU) wanaweza kuanza kutabasamu; dawa mpya na bora ya kufubaza makali ya virusi hivyo, ARV, imepatikana.


Pia Serikali itaanza kutoa ARV kila baada ya miezi mitatu kwa wagonjwa ambao afya zao zinaridhisha, kwa kwa mujibu wa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu.


Hata hivyo, watu wanaoishi na VVU watalazimika kusubiri hadi mwakani wakati Serikali itakapoanza kugawa dawa hizo.


Waziri Ummy aliyasema hayo jana wakati wa uzinduzi wa kampeni ya “Furaha Yangu, Pima, Jitambue, Ishi”. Kampeni hiyo inalenga kuhamasisha upimaji wa VVU hasa kwa wanaume na kutoa ARV kwa walioambukizwa.


Waziri Ummy alisema dawa hizo zina ufanisi zaidi na maudhi kidogo.


“Kuna maudhi katika hizi dawa wanazotumia (sasa) wenye VVU. Kwa hiyo mwakani tutatoa dawa mpya zenye ufanisi zaidi ukilinganisha na hizi za sasa. Hii inatokana na tafiti za kisayansi zinazoendelea kufanyika chini ya WHO (Shirika la Afya Duniani),” alisema.


Pia Ummy alisema Serikali imeanza majaribio ya kutoa dawa za ARV kwa miezi mitatu kwa watu ambao mwenendo wao wa matumizi ya dawa hizo unaridhisha badala ya mwezi mmoja kwa sababu kiwango cha VVU kimeshuka.


“Iwapo hali yake ya kiafya inaridhisha, haina maana kwenda kuchukua dawa kila mwezi, lakini utaratibu huu hautawahusu wanawake wajawazito, watoto chini ya miaka mitano na wale ambao hawatakidhi vigezo vya kitaalamu vilivyowekwa,” alisema.


Pia alisema katika kusogeza huduma kwa watu wanaoishi na VVU hadi kufikia Desemba, wataongeza vituo vya kutoa ushauri, kupima na kutoa dawa kutoka vituo 1,868 vilivyopo hadi 4,050. Waziri huyo alisema kati ya Sh269 bilioni zilizotengwa kununua dawa nchini, Sh5.3 bilioni ni kwa ajili ya kununua dawa za kutibu magonjwa nyemelezi.




Changamoto kwa wenye VVU


Awali mwenyekiti wa Baraza la Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (Nacopha), Justine Mwinuka alitaja changamoto zinazowakabili na kutahadharisha hatua zisipochukuliwa itarudisha nyuma mipango ya mapambano dhidi ya ugonjwa huo.


Alisema changamoto hizo ni umbali wa vituo vya afya, upatikanaji mdogo wa dawa za kutibu magonjwa nyemelezi, kutumia muda mrefu katika vituo vya matibabu na hasa kwenye mikoa yenye maambukizi makubwa ya VVU kama Njombe na Iringa.


“Changamoto nyingine ni lugha na unyanyapaa katika baadhi ya vituo vichache vya kutolea huduma na kuchelewa kutolewa kwa majibu ya vipimo vya wingi wa virusi,” alisema Mwinuka.


“Changamoto hizi zisiposhughulikiwa zitarudisha nyuma juhudi za matibabu ikiwa ndilo lengo kuu la kupima maambukizi na kujitambua.”


Akizindua kampeni hiyo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliwaagiza wakuu wa mikoa kushirikiana na wadau kufanya kampeni hiyo kwa miezi sita ili Watanzania wapate nafasi ya kupima afya zao.


“Wakuu wa mikoa nendeni kushirikiana na wadau wanaopambana na VVU kuandaa kampeni kama hizi katika maeneo yenu. Nawapeni miezi sita mfululizo ili kuwapa nafasi wananchi kupima afya zao na kuanza kutumia dawa kwa wale watakaogundulika kuwa wanaishi na VVU,” alisema Majaliwa.


Pia aliwataka wakuu hao wa mikoa kuweka mabanda yanayowawezesha watu kupima afya zao kila mahali palipo na mikusanyiko.


Mwakilishi wa Shirika la Kimataifa la Misaada la Marekani (Usaid), Andrew Karas alisema imethibitika kuwa mtu anapopima na kutambua kuwa na VVU, na kuanza kutumia dawa mapema anaweza kuishi maisha marefu.


“Mpaka sasa Watanzania walioambukizwa virusi vya Ukimwi ni asilimia 52 tu ndio wanatambua hali zao,” alisema.


“Asilimia 48 ya waliombukizwa virusi hivyo hawajui hali zao na hivyo wanakosa haki ya msingi ya kuanza matibabu. Jukumu letu ni kuelimisha na kuhamasisha kaka zetu na dada zetu kupima kujua hali zao.”


Na Sharon Sauwa, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527