Bil 2.6 KUFANYA MAPINDUZI YA VITUO SITA VYA AFYA SHINYANGA


Serikali kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI pamoja na Wizara ya Afya,maendeleo ya jamii,jinsia,wazee na watoto, Wizara fedha na mipango na wadau wa maendeleo imetoa jumla ya sh. Bil 2.6 kwa Mkoa wa Shinyanga kwa lengo la kujenga na kukarabati vituo vya Afya 6 ili vituo hivyo viweze kutoa huduma za dharura za uzazi ikiwemo upasuaji.

Akizungumza katika ziara ya ufuatiliaji wa ukarabati wa vituo hivyo,Mkurugenzi msaidizi wa Idara ya huduma za Ustawi wa jamii kutoka OR TAMISEMI Rasheed Maftaha ambaye anaongoza timu hiyo ya ufuatiliaji,amesema kuwa, Serikali imeweka mkakati madhubuti wa kuimarisha vituo vya Afya 513 nchi nzima ili viweze kutoa huduma za dharura.

Maftaha amesema Serikali imeshapeleka fedha katika vituo 44 nchi nzima ambavyo vipo katika hatua ya ukamilishaji.

Aidha, vituo vingine 139 nchini vimeshapelekewa fedha kwa ajili ya kuanza ukarabati mara moja.

Mkoa wa Shinyanga umepata sh. 2.6 bil katika vituo vya Afya 6 ambavyo ni Songwa katika Wilaya ya Kishapu kilichopata sh. Mil 400.

Katika Wilaya ya Shinyanga vituo viwili vimepokea jumla ya sh. Mil 900 ambavyo ni Samuye sh. Mil 500 naTinde sh. Mil 400, katika Wilaya ya Kahama kituo cha Chela kimepokea sh. Mil 400, Iyenze sh. Mil 500 pamoja na Ukune sh. Mil 400.

Katika awamu ya kwanza iliyotolewa mwezi Agosti mwaka jana 2017, kituo cha Afya Iyenze kilichopo Halmashauri ya Mji Kahama kipo katika hatua ya ukamilishaji, ambapo vituo vingine vya Songwa,Samuye,Tinde,Chela na Ukune vimeshaanza maandalizi ikiwemo kutenga maeneo ya ujenzi pamoja na uundaji wa kamati za kusimamia ujenzi huo kutoka kwenye uwakilishi wa wananchi. Maftaha amesema mkakati huo wa sh. 1.3 trilioni unafadhiliwa na Benki ya dunia, Serikali ya Canada pamoja na Serikali ya Denmark ni muendelezo wa utekelezaji wa mpango wa MMAM ambao kwa miaka 10 umekuwa haujatekelezwa kikamilifu.

Timu hiyo ya ufuatiliaji ipo Mkoani Shinyanga kwa siku 3 na imetembelea Wilaya zote tatu za Shinyanga, Kishapu na Kahama, kuona utekelezaji wa ukarabati wa vituo hivyo. 
Timu ya ufuatiliaji kutoka OR TAMISEMI wakiwa eneo la kituo cha Afya Iyenze ambacho kimepokea sh. Mil 500 na kipo hatua ya ukamilishaji. 
Ujenzi wa kituo cha afya Iyenze katika Halmashauri ya Kahama Mji,ukiwa hatua ya ukamilishaji. 
Timu ikiwa katika kijiji cha Songwa wakioneshwa eneo la ujenzi wa kituo baada ya kupokea sh. Mil 400. 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527