MHITIMU WA DARASA LA SABA ABAKWA,AUAWA KISHA KUTUPWA MAKABURINI


Mwili wa mtoto Lucia Thomas ambaye amefanyiwa ukatili ukiwa ndani ya Jeneza ukiagwa na kusafirishwa kwenda wilayani Bunda mkoani Mara kwa ajili ya mazishi.
Baadhi ya majirani,ndugu,jamaa na marafiki wakiwa nje kwa ajili ya kuaga mwili wa marehemu.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mkoani, Salvatory Edward akisisitiza kufungwa kwa vituo bubu vya kufundishia wanafunzi kwenye mtaa ambao anauongoza. 
Mchungaji wa Kanisa la Heri wenye moyo safi , Samwel Samson akihubiri na kutoa neno la faraja kwa familia.
Baadhi ya wananchi wakiwa kwenye hali ya masikitiko na maombolezo. Picha na Joel Maduka,Geita

***
Mtoto Lucia Thomas mwenye umri wa miaka 12 amekutwa akiwa ameuawa na mwili wake kutupwa eneo la makaburi mtaa wa mkoani mjini Geita.

Mwenyekiti wa mtaa wa Mkoani, Salvatory Edward amedai pamoja na kunyongwa hadi kufa, mwili wa mtoto huyo aliyehitimu darasa la saba mwaka huu katika Shule ya Msingi Kiandege wilayani Bunda pia ulikuwa na dalili za kubakwa kabla ya kuuawa.

Mama mkubwa wa mtoto huyo Bi, Grace Thomas amesema hata wao wameshangazwa na tukio hilo kwani mtoto huyo alikuja Geita akitokea Jijini Mwanza akiwa salama na kwamba kwa mtu ambaye ametenda ukatili huo ni vyema kwa vyombo vya sheria vikafuatilia kwa umakini hili waweze kumchukulia hatua za kisheria.

Mama Mzazi wa Mtoto huyo Bi, Mary Thomas alisema mwanaye alitoka nyumbani juzi Alhamis saa 12:30 jioni akiwa ameongozana na mtu aliyesema ni mwalimu wake wa masomo ya maandalizi ya kujiunga na kidato cha kwanza kwa maelezo kuwa anaenda kuchukua karatasi za mitihani ya somo la Uraia.

Aidha ameongeza kuwa baada ya kuona usiku umeingia bila mtoto kurejea nyumbani, alikwenda kwa mwalimu mwingine aliyemtaja kwa jina moja la ambapo waliongoza hadi nyumbani kwa mwalimu aliyeondoka na mwanaye na kumkuta lakini akawatoroka kwa kujifanya anampa mtu begi alilolishika mkononi.

Baada ya mwalimu huyo kutorejea huku mtoto haonekani, waliendelea kumtafuta mtoto wake usiku kucha bila mafanikio ndipo alipoenda kutoa taarifa polisi alikotakiwa kurejea iwapo itapita saa 24 bila mtoto kurejea nyumbani.

“Kabla ya saa 24 kumalizika, taarifa zilinifikia kuwa mwili wa mwanangu umeonekana makaburini akiwa tayari amefariki huku ukiwa na michubuko shingoni na akiwa amefungwa kamba miguuni huku hana nguo ya ndani,” alisema Bi,Mary .

Kutokana na tukio hilo, uongozi wa serikali ya mtaa wa mkoani umepiga marufuku vituo vyote vya masomo ya ziada eneo hilo na kuwataka wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao kwenye shule zinazotambulika kisheria badala ya vituo vya vichochoroni.

Imeandikwa na Joel Maduka,Geita

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527