MKAPA AKUMBUSHIA KAULI YAKE YA "WAPUMBAVU"....ADAI SASA UPUMBAVU WAO UTAPUNGUA


Rais Mstaafu awamu ya Tatu Benjamin William Mkapa amefunguka na kusema tafiti zilizotolewa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Ally Mwalimu zitawafungua kidogo wale watu aliowaita wapumbavu kipindi cha kampeni za uchaguzi.

Mhe. Mkapa amesema hayo leo alipokuwa wilayani Chato mkoani Geita wakati akikabidhi nyumba 50 zilizojengwa na taasisi yake The Benjamin William Mkapa Foundation (BMF)na kusema kwa takwimu mbalimbali zilizotolewa na waziri kwa upande wa sekta ya afya tu kunatosha kuwapunguza upumbavu watu aliowahi kuwaita wapumbavu.

"Kwa takwimu alizotoa Waziri wa Afya juu ya maendeleo ya afya nchini na mipango ya afya tu, naamini itapunguza kidogo 'Upumbavu' wa wale niliowahi kuwaita wapumbavu siku za nyuma" alisema Mkapa.

Mbali na hilo Rais mtaafu alieleza sababu kadhaa zilizomfanya kumteua kwa mara ya kwanza John Pombe Magufuli kuwa Naibu Waziri na baadaye kumteua kuwa Waziri kabisa kuwa ni pamoja na uchapaji kazi wake

"Mimi nilimteua Magufuli kuwa Naibu Waziri na baadaye kuwa waziri kutokana na utendaji wake wa kazi, nguvu zake na hali yake ya kufanya kazi, kwani alikuwa ni mtu mwenye upendo wa dhati na kujali kile anachokifanya" alisema Rais Mstaafu Benjamin Mkapa

Aidha Mkapa alisema yeye ni Rais mstaafu lakini hajastaafu kukitumikia chama chake Chama Cha Mapinduzi na kusema hawezi kuja kuondoka ndani ya CCM mpaka siku malaika wa mbinguni watakapokuja kumchukua.

"Mimi sijastaafu mapenzi ndani ya Chama changu cha CCM, nitaendelea kukitumikia chama changu mpaka siku Mungu atakaponiita, ndiyo nitaacha kukutumikia chama" alisema Benjamin Mkapa.

Rais Mstaafum Benjamin Mkapa mwaka 2015 katika uzinduzi wa kampeni za Chama Cha Mapinduzi aliwasema kuwa watu wanaojiita ni chama cha ukombozi ni wapumbavu kwani Tanzania tayari ilishakombolewa na ASP na TANU

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527