Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MKUU ONYA NGOs DHIDI YA FEDHA ZA KUANGAMIZA MAADILI, AZINDUA MFUKO WA SH MILIONI 70



Na Dotto Kwilasa, Dodoma

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ameyaka Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) nchini kutopokea fedha za ufadhili zinazoweza kuangamiza utu, maadili na misingi ya Kitanzania, akisisitiza kuwa rasilimali zinazotafutwa zinapaswa kulenga kuboresha maisha ya wananchi badala ya kuhatarisha mustakabali wa jamii.

Dkt. Mwigulu alitoa msimamo huo Novemba 27, 2026, wakati akihitimisha Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete, jijini Dodoma, akieleza kuwa mashirika hayo yanapaswa kuzingatia uzalendo, utu na maadili ya Watanzania katika utekelezaji wa shughuli zao.

 Amesema kupungua kwa fedha kutoka kwa wahisani hakupaswi kuwa sababu ya kusitisha huduma kwa jamii, bali mashirika yanapaswa kutafuta vyanzo endelevu vya mapato. “Tusipokee fedha za kutuangamiza. Tunatafuta fedha ili tulinde utu na tuboreshe ustawi wa Mtanzania, si kupata fedha zenye masharti yanayohatarisha maadili yetu, kizazi cha sasa na kijacho,” alisema.

Alisisitiza kuwa mashirika hayo yanapaswa kubuni vyanzo vipya vya mapato ndani ya nchi, kuimarisha ubia na sekta binafsi na kutumia ubunifu ili kuhakikisha huduma muhimu wanazotoa kwa jamii haziathiriki kutokana na mabadiliko ya ufadhili wa nje.

 Aidha, alieleza kuwa Serikali inatambua mchango wa NGOs katika maendeleo ya taifa na itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa utekelezaji wa mipango yao, huku akiyataka mashirika hayo kuimarisha uwajibikaji na kuzingatia sheria na maadili ya nchi.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alizindua Mfuko wa Maendeleo wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa kukabidhi hundi ya Sh milioni 70 kwa Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO), Jasper Makala. Mfuko huo unalenga kuongeza upatikanaji wa rasilimali za ndani na kuimarisha uwezo wa mashirika kuendeleza miradi na huduma zinazowanufaisha wananchi, sambamba na kupunguza utegemezi wa ufadhili wa nje.

Jukwaa hilo la sita tangu kuanzishwa kwake mwaka 2021 lilifanyika kuanzia Novemba 25 hadi 28, 2026, likiwakutanisha washiriki zaidi ya 3,500 kutoka Serikali, sekta binafsi, taasisi za fedha, washirika wa maendeleo na mashirika yasiyo ya kiserikali. Kaulimbiu yake ilikuwa “Fikra Mpya kuhusu Uendelevu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali: Ubunifu, Ubia na Upatikanaji wa Rasilimali Fedha kupitia Vyanzo vya Ndani,” ikiwa na lengo la kujadili mikakati ya kuimarisha uendelevu wa sekta hiyo.

Katika kuhitimisha jukwaa hilo, Novemba 28 ilipangwa kuwa siku ya mbio za hisani katika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma, kwa ajili ya kuchangia Mfuko wa Pamoja wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali. Shughuli nyingine zilizopangwa ni utoaji wa huduma za afya, uwajibikaji kwa jamii na maonesho ya bidhaa na shughuli za NGOs pamoja na wadau wa sekta binafsi.






Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com