Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TANZANIA KUENDELEA KUIMARISHA USHIRIKIANO WA KIKANDA


Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesisitiza dhamira ya kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kikanda, kukuza usalama wa baharini na kuendeleza maendeleo endelevu katika Ukanda wa mwambao wa Bahari ya Hindi.

Dhamira hiyo imeelezwa na Balozi wa Tanzania nchini India Mheshimiwa Anisa Mbega aliposhiriki Mkutano wa 25 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Nchi Wanachana wa Mwambao wa Bahari ya Hindi (Indian Ocean Rim Association – IORA), uliofanyika jijini New Delhi, India, Novemba 27, 2026.

Akizungumza katika Mkutano huo, Mhe. Balozi Mbega alisema Tanzania inasisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika kukabiliana na changamoto zinazojitokeza na kuendeleza maslahi ya pamoja ya nchi wanachama.

Alieleza kuwa changamoto hizo zimeathiri minyororo ya ugavi, usafirishaji wa bidhaa na shughuli za kiuchumi zinazotegemea njia salama na za uhakika za usafiri wa majini na kuongeza shinikizo katika shughuli za kiuchumi na maisha ya wananchi wanaoishi katika maeneo ya pwani na kupunguza uwezo wa nchi wanachama kugharamia vipaumbele muhimu vya maendeleo.

Alisema katika kukabiliana na changamoto hizo inabidi kuimarishwa kwa ushirikiano wa kikanda, uratibu wa hatua za pamoja, kuwa na mifumo endelevu ya upatikanaji wa fedha za maendeleo na IORA kuimarisha nafasi yake na uwezo wa kukabiliana na mahitaji na vipaumbele vinavyobadilika vya Nchi Wanachama.

Alielezea utayari wa Tanzania kuendelea kushirikiana kwa karibu na nchi wanachama kutekeleza malengo ya IORA na kujenga mwambao wa Bahari ya Hindi wenye amani, utulivu, ustahimilivu na ustawi kupitia ushirikiano jumuishi wa kikanda na utekelezaji wa hatua za pamoja.

Katika kuelekea maadhimisho ya miaka 30 ya kuanzishwa kwa IORA mwezi Machi 2027, Tanzania imesisitiza kuendelea kuzingatia Mkataba na malengo ya Jumuiya hiyo, kwa kuimarisha ushirikiano na mshikamano baina ya nchi wanachama na washirika wa majadiliano ili kujenga Ukanda wa Bahari ya Hindi wenye amani, utulivu na ustawi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com