Mtaalamu kutoka Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Bw. Paulo Joseph (kulia), akionesha vielelezo vya aina mbalimbali za kupe na mbung’o huku akitoa elimu kuhusu udhibiti wao na magonjwa wanayoeneza, yakiwemo ndigana kali inayoenezwa na kupe na nagana inayoenezwa na mbung’o, kwa wanafunzi waliotembelea banda la Wakala Novemba 27, 2026, wakati wa maonesho ya maadhimisho ya miaka 50 ya mafunzo ya tiba ya wanyama nchini Tanzania, katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Morogoro.
******************
-Wadau wajazana kujifunza kwa vitendo shughuli za Wakala
Na Daudi Nyingo – Morogoro
BANDA la Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) limegeuka darasa baada ya wadau mbalimbali kufurika kujifunza kwa vitendo kuhusu chanjo, uchunguzi wa magonjwa ya wanyama na huduma nyingine za Wakala katika siku nne za maonesho yaliyohitimishwa Novemba 27, 2026, kwenye Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Morogoro.
Maonesho hayo ya maadhimisho ya miaka 50 ya mafunzo ya tiba ya wanyama nchini Tanzania yamefanyika kuanzia Novemba 24 hadi 27, 2026. Katika kipindi hicho, wageni wamepatiwa elimu kupitia vifaa vya maabara, sampuli na vielelezo vilivyowawezesha kuoanisha maelezo ya wataalamu na shughuli zinazofanywa na TVLA.
Akielezea elimu iliyotolewa bandani, mtaalamu wa TVLA, Dkt. Jumanne Jumbe, amesema wataalamu wa Wakala wamejikita katika kuwaelimisha wadau kuhusu huduma za uchunguzi na utambuzi wa magonjwa ya wanyama, uhakiki wa ubora wa vyakula vya mifugo, pamoja na uhakiki na usajili wa viuatilifu vya mifugo.
“TVLA tumetumia vifaa, sampuli na vielelezo kuwasaidia wadau kuelewa shughuli tunazozifanya. Wanapokiona kifaa na kupata ufafanuzi wa matumizi yake, wanapata nafasi ya kuuliza maswali na kufahamu namna wanavyoweza kunufaika na huduma zetu,” amesema Dkt. Jumbe.
Katika utoaji wa elimu hiyo, TVLA imetumia vifaa vya PCR, ELISA na hadubini vilivyooneshwa bandani, pamoja na picha za vifaa vingine vya maabara. Sampuli za vyakula vya mifugo, mfano wa josho na vielelezo vya mbung’o pia vimetumika kufafanua huduma mbalimbali za Wakala.
Kwa upande wa chanjo, Afisa Mtafiti Mifugo wa TVLA, Bw. Paulo Joseph, amesema wageni wamepewa maelezo kuhusu aina saba za chanjo za mifugo zinazozalishwa na Wakala, namna zinavyosambazwa, upatikanaji na matumizi yake sahihi.
“Pamoja na kuwaonesha chanjo tunazozalisha, tumewapa wadau maelezo kuhusu upatikanaji wake na umuhimu wa kufuata maelekezo ya matumizi na utunzaji. Pia tumepokea maswali yao kuhusu maeneo wanakoweza kupata chanjo na huduma nyingine za TVLA,” amesema Bw. Paulo.
Baadhi ya wanafunzi waliotembelea banda la TVLA wamesema fursa ya kujionea vifaa na kupata maelezo kutoka kwa wataalamu imewasaidia kuhusianisha wanayojifunza darasani na shughuli za maabara, pamoja na kufahamu zaidi matumizi ya vifaa hivyo.
Kwa upande wao, baadhi ya wafugaji wameeleza kuwa elimu kuhusu chanjo, uchunguzi wa magonjwa na uhakiki wa ubora wa vyakula vya mifugo imewasaidia kufahamu huduma wanazoweza kuzipata TVLA. Pia wametaka kufahamu maeneo vilipo vituo vya Wakala nchini ili waweze kuvifikia kwa urahisi.
Maonesho hayo yameandaliwa na SUA kwa kushirikiana na Chama cha Madaktari wa Mifugo Tanzania (TVA), huku timu ya wataalamu wa TVLA ikitoa elimu kwa wahadhiri, wanafunzi, wafugaji na wadau wengine waliotembelea banda la Wakala.
Mtaalamu kutoka Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Dkt. Jumanne Jumbe (kushoto), akifafanua shughuli za uchunguzi na utambuzi wa magonjwa ya wanyama kwa wanafunzi waliotembelea banda la Wakala kujifunza kuhusu huduma za maabara, Novemba 27, 2026, wakati wa maonesho ya maadhimisho ya miaka 50 ya mafunzo ya tiba ya wanyama nchini Tanzania, katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Morogoro.
Mtaalamu kutoka Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Dkt. Jumanne Jumbe (kushoto), akitoa elimu kuhusu huduma za Wakala kwa wadau wa mifugo waliotembelea banda lake kujionea vifaa vya maabara, sampuli na vielelezo vya kufundishia, Novemba 27, 2026, wakati wa maonesho ya maadhimisho ya miaka 50 ya mafunzo ya tiba ya wanyama nchini Tanzania, katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Morogoro.
Mtaalamu kutoka Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Bw. Paulo Joseph (kushoto), akitoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya chanjo ya TEMEVAC kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) waliotembelea banda la Wakala Novemba 27, 2026, wakati wa maonesho ya maadhimisho ya miaka 50 ya mafunzo ya tiba ya wanyama nchini Tanzania, SUA, Morogoro.

Wataalamu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Bw. Paulo Joseph (kushoto) na Dkt. Jumanne Jumbe (katikati), wakitoa elimu kwa vitendo kuhusu matumizi ya vifaa vya maabara katika uchunguzi na utambuzi wa magonjwa ya wanyama kwa wadau waliotembelea banda la Wakala kujionea vifaa na vielelezo vya kufundishia, Novemba 27, 2026, wakati wa maonesho ya maadhimisho ya miaka 50 ya mafunzo ya tiba ya wanyama nchini Tanzania, katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Morogoro.










TAFUTA HABARI
Social Plugin