Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TANZANIA, CAF WASAINI MKATABA WA HAKI ZA MATANGAZO KUELEKEA AFCON 2027

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika (CAF) zimesaini Mkataba wa Haki za Matangazo kuelekea Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027), itakayofanyika kwa pamoja nchini Tanzania, Kenya na Uganda.

Mkataba huo umesainiwa leo Novemba 25, 2026, jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Dkt. Thereza Mugobi, kwa niaba ya Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, na Katibu Mkuu wa CAF, Bw. Samson Adamu.

Akizungumza kabla ya utiaji saini, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), amesema ushirikiano huo ni fursa muhimu ya kukuza sekta ya utalii na mnyororo wake wa thamani, kupitia ongezeko la wageni na shughuli mbalimbali za kiuchumi zitakazochochewa na michuano hiyo.

Amesema Serikali imejipanga kuhakikisha Tanzania inanufaika kikamilifu na AFCON 2027, kwa kutumia jukwaa hilo kuitangaza nchi na vivutio vyake vya utalii kimataifa.

Aidha, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uongozi wake na juhudi za kufungua fursa za kimataifa zinazochochea maendeleo ya sekta mbalimbali, ikiwemo utalii na michezo.

Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Makonda (Mb), amesema AFCON 2027 ni fursa kubwa ya kiuchumi kwa Tanzania, kwani inatarajiwa kuvutia wageni wengi, kuongeza shughuli za kibiashara na kupanua fursa za kipato kwa wananchi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com