Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KAMATI YA URATIBU EAC YAKUTANA KUKAMILISHA MAANDALIZI YA MKUTANO WA 48 WA BARAZA LA MAWAZIRI

Kamati ya Uratibu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imekutana Munyonyo, jijini Kampala, Uganda, kukamilisha maandalizi ya Mkutano wa 48 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya hiyo, unaotarajiwa kufanyika Novemba 30, 2026.

Mkutano huo wa Kamati ya Uratibu, unaowakutanisha Makatibu Wakuu wanaosimamia masuala ya ushirikiano wa Afrika Mashariki kutoka nchi wanachama, umejikita katika kupitia na kujadili taarifa ya wataalamu waliokutana kuanzia Novemba 23 hadi 26, 2026, kuhusu utekelezaji wa maamuzi na maelekezo yaliyotolewa katika mikutano iliyopita ya Baraza la Mawaziri.

Taarifa hiyo imejumuisha masuala mbalimbali ya kimkakati, ikiwemo hali ya utekelezaji wa maamuzi na maagizo ya Baraza la Mawaziri lililopita, ripoti ya Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya EAC, pamoja na maendeleo ya ushirikiano katika sekta za biashara, uwekezaji, miundombinu, afya, amani na usalama, masuala ya kisiasa na sekta za uzalishaji.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya EAC, Balozi Stephen P. Mbundi, amesisitiza umuhimu wa kuendeleza mshikamano na ushirikiano miongoni mwa nchi wanachama, akieleza kuwa dhamira ya pamoja ni msingi muhimu katika kuimarisha na kusukuma ajenda ya mtangamano wa kikanda kwa manufaa ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya wananchi wa Afrika Mashariki.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki ya Uganda, Bi. Edith Mwanje, ambaye ni Mwenyekiti wa mkutano huo, amesisitiza nafasi ya Kamati ya Uratibu katika kutafuta suluhisho la changamoto zinazokabili Jumuiya, kuratibu utekelezaji wa maamuzi ya kisera na kuhakikisha mapendekezo yanayotolewa yanatekelezwa kwa wakati.

Ameeleza kuwa utekelezaji madhubuti wa maamuzi ya Jumuiya ni muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kuhakikisha wananchi wananufaika na fursa zinazotokana na mtangamano wa Afrika Mashariki.

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo umeongozwa na Mkurugenzi wa Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji katika Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Benjamin Mwesiga, akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Charles Ngeleja Kadonya.

Wajumbe wengine ni Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Kijamii, Mhandisi Adillah Mataka; Mkurugenzi wa Siasa, Ulinzi na Usalama, Bi. Mwanamridu Amiry Jumaa; Mkurugenzi wa Huduma za Sheria, Bw. Elisha Suku, pamoja na maafisa waandamizi kutoka Wizara na taasisi mbalimbali za Serikali.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com