Mwigizaji mkongwe wa Nigeria, Pete Edochie, amefariki dunia Novemba 25, 2026, akiwa na umri wa miaka 79, na kuacha pengo kubwa katika tasnia ya filamu nchini Nigeria na Afrika kwa ujumla.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na familia yake kupitia mwanaye, Leo Pete Edochie, mwigizaji huyo alifariki saa 12:30 alfajiri katika jimbo la Enugu, Nigeria, baada ya kuugua saratani ya tezi dume kwa muda mfupi.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa familia imepokea msiba huo kwa huzuni kubwa, huku mipango ya mazishi ikitarajiwa kutangazwa baadaye.
Pete Edochie alikuwa miongoni mwa waigizaji wenye majina makubwa katika tasnia ya filamu ya Nigeria maarufu kama Nollywood, akipata umaarufu mkubwa kupitia uigizaji wake wa mhusika Okonkwo katika filamu ya televisheni ya Things Fall Apart ya mwaka 1987, iliyotokana na riwaya maarufu ya mwandishi wa Nigeria, Chinua Achebe.
Kabla ya kuingia kikamilifu katika tasnia ya filamu, Edochie alikuwa mtangazaji wa redio. Alianza kazi hiyo mwaka 1967 katika Shirika la Utangazaji la Nigeria Mashariki (Eastern Nigerian Broadcasting Corporation), ambako alipanda ngazi mbalimbali hadi kufikia nyadhifa za uongozi katika Shirika la Utangazaji la Anambra (Anambra Broadcasting Service).
Katika safari yake ya uigizaji, alishiriki katika filamu mbalimbali zilizopata umaarufu, zikiwemo Rituals, Billionaire’s Club na Lionheart ya mwaka 2018, ambamo aliigiza kama Chief Ernest Obiagu.
Mchango wake katika filamu, televisheni na utangazaji ulimfanya kuwa miongoni mwa watu wenye ushawishi mkubwa katika tasnia ya burudani barani Afrika. Alikumbukwa kwa sauti yake nzito na ya kipekee, busara katika uigizaji pamoja na uwezo wa kuigiza wahusika wenye mamlaka na hekima.
Kifo chake ni pigo kwa tasnia ya filamu ya Nigeria na Afrika, hasa kwa mashabiki waliovutiwa na kazi zake kwa miongo kadhaa.

EDOCHIE AFARIKI DUNIA AKIWA NA MIAKA 79
TAFUTA HABARI
Social Plugin