Shirika la World Vision Tanzania kupitia mradi wa Mwakipoya Area Programm kwa kushirikiana na GrowEnrich limeendelea kuwawezesha wananchi wa Kata ya Mwakipoya, Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, katika shughuli za kilimo, ufugaji na lishe bora kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa chakula, kuimarisha uchumi wa kaya na kuwajengea uwezo wa kujitegemea kiuchumi.
Meneja wa mradi wa GrowEnrich, Shukrani Dickson,akizungumzaia mradi huo Oktoba 22,2026 wakati wa ziara ya shirika la World Vision na ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wilayani humo amesema mradi unalenga kuimarisha lishe, kuongeza uzalishaji wa chakula na kuwasaidia wananchi kutumia fursa zilizopo katika maeneo yao kujiongezea kipato. Amesema kupitia ushirikiano na jamii, mradi umekuwa ukiwawezesha wakulima kwa kuwapatia mafunzo na nyenzo zinazosaidia kuboresha shughuli zao za uzalishaji.
Katika kuendeleza kilimo cha bustani, vikundi vya wakulima vilivyoanzishwa na wananchi na kuwezeshwa na World Vision kupitia GrowEnrich kwa kugawiwa machine 15 za kumwagilizia (Generator) na jumla kufikia 18, uwezeshaji huo unalenga kuongeza uzalishaji wa mboga kwa matumizi ya kaya na biashara,mahinci na viazi lishe ili wananchi waweze kupata chakula chenye virutubisho na kipato kutokana na mauzo ya ziada.
Akielezea matumizi ya teknolojia ya umwagiliaji katika kilimo, Afisa Kilimo Halmashauri ya Kishapu Denis Mayomba, amesema World Vision imewawezesha kutumia vifaa vya umwagiliaji aina ya "sprinkler" vinavyosambaza maji mashambani kwa mzunguko. Amesema vifaa hivyo vimeunganishwa na pampu za maji aina ya Honda zinazotumia petroli, zikiwa na uwezo wa kumwagilia ekari moja kwa takribani saa mbili, kutegemea hali ya eneo na mpangilio wa umwagiliaji. "Kiukweli teknolojia hii inasaidia kupunguza muda na nguvu zinazotumika kumwagilia, huku ikiboresha ufanisi wa uzalishaji wa mazao" ameongeza Mayomba.
Kwa upande wake, Stanslaus Magomasi mkazi wa Mwakipoya ambaye ni mkulima wa mahindi na viazi lishe, amesema kilimo hicho kina manufaa makubwa kwa familia kwa sababu kinasaidia upatikanaji wa chakula na kuongeza kipato kupitia mauzo ya mazao.
Amesema, “Kilimo cha mahindi lishe na viazi lishe kinatusaidia kupata chakula kwa ajili ya familia zetu na kuhakikisha tunapata vyakula vyenye virutubisho. Tunapopata mavuno ya ziada, tunauza na kutumia fedha hizo kugharamia mahitaji mengine ya nyumbani. Hii inatusaidia kupunguza gharama za kununua chakula na kuimarisha uchumi wa familia zetu.” ameongeza Stanslaus
Katika shughuli nyingine za uwezeshaji, vikundi vinane vya ufugaji vimewezeshwa kufuga mbuzi, vikiwa na jumla ya wanachama 152, huku vikundi vitatu vya wafugaji nyuki katika vijiji vya Mwangongo, Iboja na Mwakipoya vikinufaika na mizinga 72 kutoka World Vision., Aidha, vikundi 16 vya wakulima vyenye wanachama 192 vimepata fursa za kuimarisha shughuli za kilimo, ikiwemo uzalishaji wa viazi lishe na mahindi lishe.
Katika eneo la afya na lishe
"Kwa sasa tumewafikia wananchi wengi sana kwenye mfumo huu wa Mkoba na tayari tunaona matokeo kwa wanawake wajawazito na watoto chini ya miaka mitano afya zake zinaendelea kuimarika tayari wanafahamu umuhimu wa kuhudhuria mapema kliniki na kuchunguza afya ya mama na baba ili kumkinga mtoto aliyeko tumboni, kunyonyesha mtoto kwa miezi sita bila kumpa chakula cha ziada na kunyonyesha miaka miwili mfululizo pamoja na kujenga vyoo bora na kuvitumia" amesema Mhudumu ngazi ya jamii Jonh Andrew Gungutu mhudumu wa afya ngazi ya jamii
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Badi Shabani Kangomba, amesema elimu kuhusu lishe bora, matumizi ya vyakula vyenye virutubisho na umuhimu wa mlo kamili ni muhimu katika kuboresha afya za wananchi. Ameeleza kuwa ushirikiano na miradi ya maendeleo unasaidia kuongeza uelewa wa jamii kuhusu namna ya kutumia vyakula vinavyopatikana katika mazingira yao kuboresha lishe ya familia.
Diwani wa Kata ya Mwakipoya Mhe. Tabitha Sadikiel Mbango amepongeza juhudi za Serikali kwa kuendelea kukaribisha wadau mbalimbali na kuwafikia wananchi hasa wa Vijijini na kuwaboreshea mazingira wananchi, huku akiwataka wanakikundi kuendelea kuwa wamoja na kutumia nafasi hiyo adhimu kwa masilahi mapana ya kujiinua kwani itawasaidia kupata nafasi ya kuchukua mikopo ya asilimia 10 inayotolewa bila liba na serikali kupitia Halmashauri.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Tano Malele, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo katika kuwajengea wananchi uwezo wa kiuchumi. Amesema uwezeshaji wa wananchi kupitia mafunzo, vifaa na fursa za uzalishaji unawasaidia kujitegemea, kuongeza kipato na kuboresha maisha yao kwa muda mrefu.
Tano ameutaka uongozi wa Kijiji cha Badi kuhakikisha wanashirikiana na wananchi kupata fedha ili wakarabati jengo la huduma za mama na mtoto huku World Vision ikiahidi kuongeza nguvu katika maboresho hayo.
Kwa ujumla, utekelezaji wa mradi huo kupitia GrowEnrich unaonesha umuhimu wa kuwawezesha wananchi kutumia kilimo na ufugaji kama nyenzo za kuboresha lishe na kuimarisha uchumi wa kaya. Ushirikiano kati ya World Vision Tanzania, Serikali na vikundi vya wananchi ni muhimu katika kuhakikisha ujuzi na fursa zinazotolewa zinatumika kwa tija na kuleta maendeleo endelevu katika Wilaya ya Kishapu.
Mratibu wa mriadi ya maendeleo Lagana na Mwakipoya (AP), WorldVision wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga Yohana Masanja
Meneja Mradi wa Grow Enrich Shukran Dickson
Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Mwita Mwijarubi
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Badi Shabani Kangomba
Mkazi wa Kata ya Mwakipoya wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga ambaye pia ni mkulima wa mahindi na viazi lishe akielezea namna alivyonufaika na mradi huo wa Mwakipoya (AP) Clement Mgema
TAFUTA HABARI
Kamusi
Social Plugin