Mradi wa maji safi na salama kutoka Ziwa Victoria Kata ya Mwakipoya wilayani Kishapu, mkoani Shinyanga, uliotekelezwa na Shirika la WorldVision wenye gharama ya shilingi milioni 79.38
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoni Shinyanga ambaye ni Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya jamii Joseph Swalala
Na Sumai Salum – Kishapu
Wananchi 1,744 wa Kijiji cha Iboja, Kata ya Mwakipoya wilayani Kishapu, mkoani Shinyanga, wamenufaika na mradi wa maji safi na salama kutoka Ziwa Victoria, mradi uliotekelezwa na Shirika la WorldVision wenye gharama ya shilingi milioni 79.38 kwa lengo la kuokoa maisha, kupunguza adha ya kutafuta maji na kuboresha afya za wananchi.
Akizungumza Oktoba 22,2026 wakati wa ziara ya serikali ya Wilaya na Shirika hilo, Mratibu miradi ya maendeleo Lagana Mwakipoya (Area Program) Yohana Masanja amesema Mradi huo unahusisha mtandao wa mabomba wenye urefu wa kilomita 7.9 kutoka chanzo cha maji kupitia tanki la Mwangongo, ukiwa na vituo vinne vya kuchotea maji, viwili kwa ajili ya taasisi zikiwemo Shule na Zahanati, na viwili vya matumizi ya jamii huku baadhi ya Wananchi kutoka maeneo ya jirani pia wamekuwa wakinufaika na mradi huo.
Utekelezaji wa mradi huo ulitokana na uhitaji wa maji katika eneo hilo, huku changamoto ya upatikanaji wa maji ikihusishwa na hatari kwa maisha ya wananchi ambapo mwaka 2024, kifo cha mwanafunzi wa kidato cha pili kilikuwa miongoni mwa matukio yaliyosisitiza umuhimu wa kutafuta suluhisho la changamoto hiyo ikiwa ni pamoja na magonjwa na kuimarisha usalama wa wananchi likiwa ni ombi la jamii kwa World Vision.
Aidha katika Kijiji cha Mwakipoya Shirika hilo limechimba na sasa mradi unatumika kisima kirefu chenye urefu wa Km 8.2 mradi wenye thamani ya Tsh. milioni 223 ikiwa ni pamoja na uchimbaji mitaro, kulaza bomba na kufukia, ujenzi wa tank (lita 50,000),ujenzi wa pump house, mfumo wa umeme wa Tanesco na Sola pamoja na uzio.
Chanzo cha maji ya kishima kirefu Kijiji cha Mwakipoya
"Wanufaika wa mradi huu ni jumla ya wananchi 3388 kutoka kwenye Kaya 482 kukiwa na chanzo kimoja na vituo 8 huku vitatu vikiwa kwenye Taasisi Zahanati Shuleni na Msikitini na vingine vitano vikiwa kwenye jamii" ameongeza Masanja
Mhandisi kutoka RUWASA wilayani Kishapu Jonh Lugembe amesema kisima hicho kinazalisha maji lita 3600 kwa saa moja na hadi sasa jumla ya kaya 8 zimesogezewa huduma hiyo majumbani.
Meneja wa Shirika la World Vision Tanzania Kanda ya Ziwa, Goodluck Nnko, amesema shirika hilo linalenga kushirikiana na Serikali na jamii kutekeleza miradi inayoboresha maisha ya wananchi, hususan katika upatikanaji wa huduma za maji safi na salama, afya, lishe, elimu na uwezeshaji wa kiuchumi.
"World Vision inaendelea kuelekeza nguvu zake katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi kwa kuimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali, ili kuhakikisha miradi inayotekelezwa inaleta matokeo chanya na endelevu kwa jamii" Amesisitiza Nnko.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, mwakilishi wake, Tano Malele, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, wadau wa maendeleo na wananchi katika kutekeleza miradi inayogusa maisha ya watu. Amesema miradi ya maji ina thamani kubwa kwa kuwa inalinda uhai, hupunguza mazingira hatarishi na kusaidia kuzuia magonjwa yanayotokana na matumizi ya maji yasiyo salama.
Aidha, amewahimiza wananchi kulinda na kutunza miundombinu ya miradi hiyo ili iweze kudumu na kuendelea kutoa huduma ikilinganishwa na hatua za awali za utekelezaji wa mradi, kulikuwa na changamoto ya wizi wa mabomba, na baadae yakapatikana. Hivyo, wananchi wametakiwa kuwa walinzi wa miundombinu ya maendeleo inayowekwa katika maeneo yao.
Mbali na mradi wa maji, World Vision Tanzania kwa kushirikiana na wadau wengine imeendelea kutekeleza shughuli za maendeleo katika Kata ya Mwakipoya kupitia miradi mbalimbali wakishirikiana na KIVULINI,Grow Enrich unaolenga kuimarisha uchumi wa kaya, uzalishaji, afya, lishe, elimu na ulinzi wa watoto na watu wazima.
Katika sekta ya ufugaji, vikundi vinane vimewezeshwa kufuga mbuzi, ambapo kila kikundi kina wanachama 19 na kunufaisha jumla ya watu 152. Pia, vikundi vitatu vya wafugaji nyuki katika vijiji vya Mwangongo, Iboja na Mwakipoya vimewezeshwa mizinga 72, huku uzalishaji wa asali ukiendelea.
Katika kilimo, vikundi 16 vyenye wanachama 192 vimepatiwa fursa za uwezeshaji, zikiwemo vipando 2,000 vya viazi lishe, pamoja na mbegu za mahindi lishe. Wakulima 216 wamepatiwa mbegu za mahindi za chotara na kushiriki katika kilimo cha mfano, huku taarifa za utekelezaji zikionesha matokeo ya kuridhisha. Uzalishaji wa mahindi lishe na viazi lishe umechangia kuimarisha upatikanaji wa chakula katika kaya zinazofikiwa na mradi.
Mradi pia umewezesha uwekaji wa vifaa vya kunawia mikono katika Shule ya Msingi Ilula na kuhamasisha ujenzi wa vyoo bora, ambapo vyoo 67 vimejengwa. Hatua hizo zinalenga kuimarisha usafi na kuzuia magonjwa, hususan kipindupindu. Katika sekta ya elimu, mradi umeendelea kufuatilia na kuunga mkono mahitaji ya shule katika Kata hiyo kwa kuunga mkono lishe mashuleni pamoja na ugawaji madawati.
Pamoja na mafanikio hayo, bado kuna mahitaji yanayopaswa kupewa kipaumbele, ikiwemo upatikanaji wa maji katika Kijiji cha Ngeme na huduma za zahanati katika vijiji vya Iboja na Mwangongo. Pia, kuna mipango ya kupanua huduma za maji katika maeneo ya Ngeme na Ijimija ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata maji ya uhakika.
Ushirikiano kati ya Serikali, World Vision Tanzania na jamii unaendelea kuwa nyenzo muhimu katika kuboresha huduma za kijamii na kuinua uchumi wa kaya. Utunzaji wa miradi iliyotekelezwa, pamoja na kuendeleza maeneo ambayo bado yana changamoto, ni hatua muhimu katika kuhakikisha wananchi wa Kishapu wanapata huduma bora na maisha yenye ustawi.
TAFUTA HABARI
Kamusi
Social Plugin