Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

STAMICO YAONGEZA MAPATO HADI SH BILIONI 147.8


SHIRIKA la Madini la Taifa (STAMICO) limesema limeongeza mapato yake kutoka Sh bilioni 1.3 kwa mwaka 2018/19 hadi Sh bilioni 147.8 katika mwaka 2025/26, likieleza kuwa mafanikio hayo yametokana na mageuzi ya kiutendaji, uwekezaji katika miradi ya kimkakati na kuimarisha ushiriki wa Watanzania katika sekta ya madini.

Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. CPA Venance Mwasse, amesema hayo wakati akizungumza katika kikao kazi kati ya shirika hilo na wahariri wa vyombo vya habari, ambapo alieleza mikakati na mafanikio ya shirika pamoja na mipango ya kuongeza mchango wake katika uchumi wa taifa.

“Wakati tunaingia, mapato ya ndani ya shirika yalikuwa Sh bilioni 1.3 kwa mwaka mzima. Leo hii tunapozungumza, kwa hesabu zinazomalizika mwaka 2025/26, mapato yote ni Sh bilioni 147.8,” amesema Mwasse.

Amesema shirika hilo ambalo awali lilikuwa likitegemea fedha za Serikali kwa asilimia 89, sasa limeweza kujitegemea katika kulipa mishahara ya wafanyakazi wake, huku likiendelea kuchangia mapato ya Serikali kupitia gawio.

“Kwa sasa huu ni mwaka wa nne tangu tuache kutegemea Serikali, na huu ni mwaka wa tatu tunajilipa wenyewe mishahara. Tangu shirika lianzishwe mwaka 1972, tumekuwa na faida na kutoa gawio kwa Serikali, ambapo hadi sasa tumeshatoa Sh bilioni 11,” amesema.

Mwasse amesema STAMICO pia imewekeza katika miradi ya kimkakati ikiwemo uchorongaji wa miamba kwa ajili ya utafiti wa madini, ambapo idadi ya mitambo imeongezeka kutoka mitatu hadi 18 ya kisasa, huku shirika likihudumia wateja mbalimbali katika sekta hiyo.

Ameitaja miradi mingine kuwa ni uzalishaji wa nishati safi ya kupikia inayotokana na makaa ya mawe kupitia bidhaa ya Rafiki Briquettes, akieleza kuwa shirika lina viwanda vitano na limekamilisha kiwanda kipya kikubwa kuliko vingine katika Afrika Mashariki na Kati.

Amesema bidhaa hiyo inalenga kupunguza matumizi ya kuni na mkaa unaotokana na ukataji wa miti, huku akiwataka wananchi na wadau wa habari kushirikiana kuitangaza ili kuongeza matumizi yake.

“Tunataka watu waache kukata miti na watumie bidhaa inayotokana na rasilimali ya kwao, ambayo ni makaa ya mawe,” amesema Mwasse.

Aidha, amesema STAMICO imejipanga kuendeleza mradi wa makaa ya mawe wa Mchuchuma ili kurejesha umuhimu wake katika uzalishaji wa makaa ya mawe na umeme, akieleza kuwa mradi huo unalenga kuwa wa kielelezo katika maendeleo ya taifa.

Katika kuwawezesha wachimbaji wadogo, Mwasse amesema shirika limewekeza katika mitambo ya utafiti na uchimbaji, mafunzo ya kitaalamu na teknolojia zinazosaidia kuongeza uzalishaji na kupunguza upotevu wa madini.

Amesema changamoto zilizokuwa zikiwakabili wachimbaji wadogo ni pamoja na ukosefu wa taarifa za kijiolojia, teknolojia duni, mitaji na ugumu wa kupata masoko, hali iliyolifanya shirika kuandaa mikakati ya kuwaunganisha na taasisi za fedha pamoja na wanunuzi wa madini.

“Katika uchimbaji bila kujua madini yako wapi, utapata shida kubwa sana. Utapoteza mtaji na muda. Ndiyo maana tuliamua kuwasaidia wachimbaji wadogo kwa kuwapatia teknolojia za utafiti na kuwaunganisha na taasisi za fedha,” amesema.

Ameongeza kuwa STAMICO imesaini hati za makubaliano na benki mbalimbali zikiwemo Azania, CRDB na NMB kwa lengo la kuongeza fursa za mikopo kwa wachimbaji wadogo, huku mchakato wa kuanzisha Benki ya Wachimbaji Tanzania ukiendelea.

Mwasse amesema shirika pia linaendelea kutoa mafunzo kwa wachimbaji wadogo na kuanzisha vituo vya mfano vya uchimbaji ili kuhamasisha matumizi ya teknolojia salama na rafiki kwa mazingira, ikiwemo kupunguza matumizi ya zebaki katika uchenjuaji wa dhahabu.

Katika hatua nyingine, amesema STAMICO imeanzisha kiwanda cha kisasa cha kuongeza thamani ya chumvi katika Wilaya ya Kilwa, Mkoa wa Lindi, kwa lengo la kuwasaidia wazalishaji wa chumvi katika mikoa ya kusini kupata teknolojia, huduma za uchakataji na masoko.

Amesema shirika hilo pia linashiriki katika miradi ya ubia na wawekezaji katika madini ya dhahabu, nikeli na madini mengine ya kimkakati, huku likiendelea kutekeleza jukumu la Serikali la kuongeza thamani ya rasilimali za madini nchini.

Mwasse ameeleza kuwa mafanikio hayo yanaenda sambamba na ongezeko la ajira, uwekezaji na mchango wa wachimbaji wadogo katika mapato yatokanayo na sekta ya madini.

Amesema kwa mujibu wa tathmini ya mwaka wa fedha 2021/22, mchango wa wachimbaji wadogo katika mapato ya sekta ya madini uliongezeka kutoka asilimia tatu hadi asilimia 40, akieleza kuwa ongezeko hilo linaonesha umuhimu wa kuwawezesha Watanzania kushiriki katika uvunaji wa rasilimali zao.

Akizungumzia mipango ya baadaye, Mwasse amesema STAMICO imejipanga kuanzisha migodi mikubwa mitatu, miwili ya dhahabu na mmoja wa almasi, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuongeza uzalishaji na kuimarisha nafasi ya shirika katika sekta ya madini.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amelitaka shirika hilo kuendelea kuwekeza katika utafiti, ubunifu na matumizi ya takwimu za kisasa ili kuongeza tija na kuimarisha mchango wa sekta ya madini katika uchumi wa taifa.

Balile amesema mafanikio ya STAMICO yanapaswa kuambatana na utafiti endelevu unaozingatia mabadiliko ya teknolojia na mazingira ya biashara, badala ya kutegemea takwimu za miaka iliyopita wakati sekta inaendelea kubadilika.

Amesema kuongeza thamani ya madini kupitia uchimbaji, uchakataji na upatikanaji wa masoko kunaweza kuongeza ajira kwa vijana na mapato ya ndani na fedha za kigeni.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha uwajibikaji katika taasisi za umma, akieleza kuwa STAMICO inapaswa kuendelea kuweka mkazo katika matokeo, matumizi sahihi ya muda na utekelezaji wa majukumu kwa ufanisi.

Balile pia ameitaka STAMICO kuimarisha ushirikiano na wahariri na waandishi wa habari ili kuwezesha umma kupata taarifa sahihi kuhusu mafanikio, changamoto na fursa zilizopo katika sekta ya madini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com