
Serikali na wadau katika sekta ya michezo nchini wametakiwa kuongeza uwekezaji katika mchezo wa Pickleball ili kuukuza, kuutangaza na kuufanya utambulike zaidi nchini, sambamba na kuibua vipaji na kuongeza fursa za ajira kwa vijana.
Rai hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam na wachezaji pamoja na waamuzi wa mchezo huo wakati wa mashindano ya Smash and Save, yaliyoandaliwa na Rotary Dar es Salaam kwa lengo la kukusanya fedha zitakazosaidia upatikanaji wa madawati katika shule mbalimbali.
Akizungumza wakati wa mashindano hayo yaliyofanyika juzi katika viwanja vya Tanzanite, vilivyopo Mikocheni, wadau hao wamesema Tanzania imeanza vizuri katika mchezo huo tangu ulipoanza kutambulishwa rasmi nchini miaka ya hivi karibuni, huku wakieleza kuwa kuna mwitikio mkubwa kutoka kwa vijana.
Mdau, mdhamini na mchezaji wa Pickleball nchini, Dkt. Sajad Habib Rai, amesema Tanzania ina vipaji vingi vinavyoweza kufanya vizuri katika mchezo huo, akisisitiza kuwa kinachohitajika ni kuwapa vijana wanaojihusisha nao fursa na usaidizi unaostahili.
“Ukweli ni kwamba Pickleball imekuja kwa kasi hapa nchini. Ukiangalia katika viwanja mbalimbali ambako mchezo huu unachezwa, utaona mwamko mkubwa wa vijana. Watu wana moyo na mapenzi na mchezo huu. Kinachohitajika ni kuwashika mkono ili kuwa na wachezaji bora watakaoliwakilisha taifa katika michuano mbalimbali ya mchezo huo,” amesema Dkt. Sajad.
Ameongeza kuwa, kama mdau wa mchezo huo, amekuwa akijitolea kufadhili juhudi za vijana wanaopenda kuucheza, ikiwemo kuandaa mashindano maalumu yenye lengo la kuibua na kukuza vipaji.
Dkt. Sajad ameiomba Serikali, hususan Wizara yenye dhamana ya michezo, kuangalia namna bora ya kuwafikia wachezaji wa Pickleball na kuweka mikakati itakayosaidia kukuza mchezo huo na kuibua vipaji vinavyoweza kulitangaza taifa katika mashindano ya kimataifa.
Kwa upande wake, mwamuzi wa mchezo huo, Mohammed Raajan, ambaye Agosti mwaka huu alikwenda nchini Vietnam na kuchezesha fainali za dunia za Pickleball, amesema Tanzania ina uwezo wa kufanya vizuri katika mchezo huo iwapo itaweka mikakati madhubuti ya kuukuza.
Raajan amesisitiza umuhimu wa Serikali na wadau kuwekeza katika ujenzi wa viwanja maalumu vya Pickleball ili kurahisisha upatikanaji wa maeneo ya kuchezea na kuhamasisha watu wengi zaidi kushiriki mchezo huo.
Naye Kocha wa Pickleball nchini, Abdallah Manyua, amesema Tanzania ina nafasi ya kufikia mafanikio makubwa katika mchezo huo, ikiwemo kushindana kuwania ubingwa wa dunia, iwapo uwekezaji utaongezwa na wadau pamoja na wadhamini wataona umuhimu wa kuunga mkono maendeleo yake.
Amesema ushirikiano kati ya Serikali, wadau wa michezo, makampuni na wadhamini ni muhimu katika kuweka mazingira yatakayowawezesha wachezaji kupata mafunzo, kushiriki mashindano na kujiandaa kwa ushindani wa kimataifa.




Social Plugin