
Na Bora Mustafa,Arusha
VIJANA na wanawake nchini wametakiwa kutumia vipaji vyao katika sanaa na ubunifu kama fursa ya kujiajiri, kuongeza kipato na kuchangia maendeleo ya familia na jamii.
Wito huo umetolewa Jumatano, Oktoba 7, 2026, na Mkurugenzi Msaidizi wa Sanaa za Ufundi kutoka Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Bona Leoni Masenge, wakati akizungumza katika Tamasha la Arusha Arts and Festival linaloendelea jijini Arusha.
Masenge amesema sanaa na ubunifu vina uwezo mkubwa wa kuzalisha ajira na kujenga biashara, hivyo kuwataka vijana kutoviona vipaji vyao kama burudani pekee, bali kuvitumia kama fursa za kuanzisha na kukuza shughuli za kiuchumi.
Amesema mtu anayeshona, kufuma, kuchonga, kuchora, kutengeneza bidhaa za ngozi au kubuni mavazi si fundi pekee, bali ni mjasiriamali na mbunifu mwenye uwezo wa kujenga biashara yenye tija.
“Msione sanaa na ubunifu kama burudani pekee. Kipaji kinaweza kuwa biashara, ubunifu unaweza kuwa ajira na teknolojia inaweza kuwa soko,” amesema Masenge.
Kwa upande wa wanawake, Masenge amesema Serikali inataka kuona wakitumia sanaa, ubunifu na vikundi vya uzalishaji kujikwamua kiuchumi, huku akiwataka wabunifu kutumia fursa za mitaji, masoko, teknolojia na mafunzo zinazotolewa na Serikali pamoja na wadau mbalimbali.
Amesema wasanii na mafundi wa sanaa wanapaswa kusajiliwa BASATA ili kutambulika rasmi na kupata fursa mbalimbali zinazotolewa na taasisi hiyo na wadau wengine.
Ametaja pia Mfuko wa Utamaduni na Sanaa kuwa miongoni mwa fursa zinazoweza kutumiwa na wasanii na wabunifu wenye sifa kupata mitaji na kuendeleza shughuli zao.
Akizungumzia Tamasha la Arusha Arts and Festival, Masenge amesema tamasha hilo linatoa fursa kwa wasanii, mafundi na wabunifu kujenga mitandao, kufanya biashara na kuwaunganisha wazalishaji na wanunuzi pamoja na wawekezaji, hususan kupitia biashara kati ya biashara (B2B).
Aidha, amewataka vijana na wanawake kutumia teknolojia mpya, ikiwemo akili bandia (AI), katika kuboresha bidhaa na huduma zao pamoja na kufikia masoko mapana zaidi ndani na nje ya nchi.
Pamoja na hayo, amewataka Watanzania kuunga mkono bidhaa zinazozalishwa nchini kwa kuzinunua na kuzitangaza, akisema hatua hiyo itasaidia kuongeza ajira, kipato na kuchochea maendeleo ya taifa.
AJENDA YA MIAKA MITANO YA UCHUMI WA UBUNIFU
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Tourism Festival, Ibrahim Othman, amesema Tanzania imezindua Ajenda ya Kitaifa ya Maendeleo ya Mafundi na Uchumi wa Ubunifu ya Miaka Mitano, inayolenga kuweka mazingira bora kwa mafundi na wasanii kukuza shughuli zao, kuongeza fursa za ajira na kuchangia katika maendeleo ya uchumi wa nchi.
Amesema ajenda hiyo inalenga kuimarisha sekta ya ufundi na ubunifu kwa kuweka mikakati itakayowawezesha vijana na wadau wengine kutumia vipaji, ujuzi na ubunifu wao kama fursa za kiuchumi.
Kwa mujibu wa Othman, ajenda hiyo pia inalenga kuongeza upatikanaji wa mafunzo, teknolojia na masoko kwa mafundi na wabunifu, pamoja na kuwawezesha kutumia ujuzi wao kutengeneza bidhaa na huduma zinazokidhi mahitaji ya soko.
Amesema ushirikiano kati ya wadau mbalimbali ni muhimu katika kufanikisha utekelezaji wa ajenda hiyo, ikiwemo sekta binafsi, taasisi za mafunzo na wadau wa ubunifu.
Hata hivyo, pamoja na fursa zilizopo, mafundi na wasanii wamehimizwa kuendelea kuongeza ubora wa bidhaa na huduma zao, kuzingatia matumizi ya teknolojia na kuwa wabunifu ili waweze kushindana katika soko la ndani na la kimataifa.
Ajenda hiyo ya miaka mitano inatarajiwa kuwa chachu ya kuongeza thamani ya kazi za mafundi na wabunifu, kukuza ajira kwa vijana na kuimarisha mchango wa uchumi wa ubunifu katika maendeleo ya Taifa.

Social Plugin