Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BRELA YAWAHAMASISHA WASANII KURASIMISHA NA KUKUZA BIASHARA ZAO



Na Bora Mustafa,
Arusha

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umewahamasisha wasanii kurasimisha shughuli zao za kibiashara kwa kuzisajili na kuzingatia taratibu za kisheria ili waweze kunufaika na fursa mbalimbali zinazotolewa kwa wafanyabiashara waliosajiliwa.

Msaidizi wa Msajili Mkuu, Mkurugenzi wa Miliki Bunifu kutoka BRELA, Nassoro Mtavu, amesema taasisi hiyo imejipanga kuwasaidia wasanii kuelewa na kutekeleza taratibu za usajili wa biashara pamoja na masuala mengine yanayohusiana na shughuli zao.

Mtavu ameyasema hayo Oktoba 7, 2026, wakati akizungumza na wadau wa sanaa katika Tamasha la Arusha Artisan Festival linaloendelea katika viwanja vya General Tyre, Njiro jijini Arusha.

Amesema ushiriki wa BRELA katika maonyesho hayo ni sehemu ya kutoa elimu kwa wasanii na wafanyabiashara kuhusu umuhimu wa kurasimisha shughuli zao, pamoja na kuwapa fursa ya kupata ufafanuzi wa moja kwa moja kutoka kwa wataalamu wa taasisi hiyo.


“Maonyesho haya yamekuwa fursa muhimu kwa wasanii na wafanyabiashara kupata elimu kuhusu namna ya kuendesha na kukuza shughuli zao kwa kuzingatia taratibu za kisheria. Wadau wa sanaa tumieni nafasi hii kuuliza maswali kuhusu changamoto zinazowakabili katika shughuli zenu za kila siku,” amesema Mtavu.

Amesema wasanii wanapaswa kutumia fursa hiyo kueleza changamoto zinazowakabili katika shughuli zao ili waweze kupata majibu na ufumbuzi kutoka kwa wataalamu wa masuala ya usajili wa biashara, majina ya biashara, alama za biashara, miliki bunifu na maeneo mengine yanayosimamiwa na BRELA.

Vilevile, Mtavu amewahimiza wasanii kutumia fursa hiyo kujifunza zaidi kuhusu huduma zinazotolewa na BRELA, akieleza kuwa uelewa wa masuala ya usajili na ulinzi wa miliki bunifu unaweza kuwasaidia kurasimisha, kulinda na kukuza shughuli zao kwa ufanisi.
Amesema wasanii wanapaswa kuona kazi zao kama biashara na kuchukua hatua za kuzirasimisha ili kuongeza fursa za ukuaji na ushindani katika soko.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com