Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Mkoa wa Shinyanga, Amina Mdabi, amesema mfuko huo umeendelea kuboresha huduma kwa wanachama, waajiri na wastaafu kupitia matumizi ya mifumo ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA), hatua iliyosaidia kupunguza wastani wa muda wa kulipa mafao kutoka siku 63 hadi siku 19.
Mdabi ameyasema hayo Oktoba 9, 2026, wakati wa kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja 2026 yaliyofanyika mkoani Shinyanga, yenye kaulimbiu ya “Huduma Bora kwa Vitendo.”
Amesema NSSF inaendelea kuimarisha mifumo ya utoaji huduma ili kuwawezesha wanachama kupata huduma kwa urahisi, kwa wakati na kwa ufanisi zaidi, bila kulazimika kufika mara kwa mara katika ofisi za mfuko huo.
Ameeleza kuwa kupitia Lango la Huduma za NSSF (NSSF Portal), waajiri, wanachama na wastaafu wanaweza kujisajili, kufuatilia taarifa za michango, kufungua na kufuatilia madai ya mafao pamoja na kufanya uhakiki wa wastaafu kwa njia ya kidijitali.
Kwa mujibu wa Mdabi, thamani ya mfuko imeongezeka kutoka Sh trilioni 9.84 katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 2025 hadi Sh trilioni 11.4 kufikia Juni 30, 2026.
Aidha, idadi ya wanachama imeongezeka kutoka 1,616,026 Juni 2025 hadi 2,144,906 Juni 2026, sawa na ongezeko la takribani asilimia 33.
Ongezeko hilo linaonesha kupanuka kwa wigo wa hifadhi ya jamii nchini, ikiwemo kuwafikia wananchi waliojiajiri kupitia Skimu ya Hifadhi.
Katika hatua nyingine, Mdabi amewahimiza wanachama kufuatilia taarifa zao za michango na kutoa taarifa kwa NSSF wanapobaini changamoto au kutokuwapo kwa michango yao, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kulinda haki zao za kupata mafao kwa wakati.
Pia, amewataka waajiri, hususan wa sekta binafsi, kutimiza wajibu wao wa kisheria kwa kuwasilisha michango ya wafanyakazi kwa wakati kila mwezi.
Amesema NSSF inaendelea kutekeleza mpango wa msamaha wa tozo kwa waajiri watakaolipa madeni yote ya michango ya msingi na kuendelea kuwasilisha michango kwa wakati hadi Desemba 31, 2026.
Kwa upande wa utoaji huduma, amesema mfuko utaendelea kuzingatia misingi ya uadilifu, uwajibikaji, ushirikiano, weledi na utu ili kuhakikisha kila mwanachama, mwajiri na mstaafu anapata huduma inayostahili.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mgeni rasmi Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Salum Kitumbo, amewataka waajiri kuzingatia sheria kwa kuhakikisha michango ya wafanyakazi wao inawasilishwa kwa wakati ili kulinda maslahi yao, hasa wanapofikia umri wa kustaafu na kuhitaji kupata mafao yao.
Kitumbo pia amewataka watumishi wa NSSF kuendelea kutoa huduma kwa weledi, kusikiliza mahitaji ya wateja na kuhakikisha changamoto zinazowasilishwa zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati.
Baadhi ya wanachama na wawakilishi wa waajiri walioshiriki maadhimisho hayo wameeleza kuridhishwa na maboresho ya utoaji huduma katika mfuko huo, wakibainisha kuwa hatua hizo zimesaidia kupunguza usumbufu na kurahisisha upatikanaji wa huduma.
Julieth Mazumila, mwanachama wa NSSF, Nickson George, mwakilishi wa kampuni ya Jambo Group, na William Lameck, mwalimu mkuu wa Shule ya Balina, ni miongoni mwa washiriki walioeleza uzoefu wao kuhusu huduma za mfuko huo.
Maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uhusiano kati ya NSSF na wadau wake, kusikiliza maoni ya wateja na kutambua maeneo yanayohitaji maboresho ili kuhakikisha huduma za hifadhi ya jamii zinatolewa kwa ufanisi na kwa kuzingatia mahitaji ya wanachama.
Meneja wa NSSF Mkoa wa Shinyanga, Amina Mdabi, akizungumza Oktoba 9,2026 wakati wa kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja 2026 yaliyofanyika katika Ofisi za NSSF Mkoa wa Shinyanga.
Meneja wa NSSF Mkoa wa Shinyanga, Amina Mdabi, akizungumza Oktoba 9,2026 wakati wa kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja 2026 yaliyofanyika katika Ofisi za NSSF Mkoa wa Shinyanga.

Meya wa Manispaa ya Shinyanga Salum Kitumbo akizungumza Oktoba 9,2026 wakati wa kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja 2026 yaliyofanyika katika Ofisi za NSSF Mkoa wa Shinyanga.


































































Social Plugin