Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAHAFALI YA 20 KISHAPU SEKONDARI, NANGI WA UVCCM ACHANGIA MASHINE YA KUDURUFU

Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Jenipha Nangi akizungumza wakati akiwa mgeni rasmi katika Mahafali ya 20 ya Kidato cha Nne ya Shule ya Sekondari Kishapu yaliyofanyika Oktoba 9,2026


Na Sumai Salum-Kishapu


Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Jenipha Nangi, ameunga mkono jitihada za Serikali katika kuboresha sekta ya elimu kwa kuchangia vifaa vya michezo kwa Shule ya Sekondari Kishapu na kuahidi kutoa mashine ya kudurufu (photocopy machine) ili kurahisisha maandalizi ya mitihani na nyaraka mbalimbali za shule hiyo.


Nangi ametoa msaada huo leo Oktoba 9, 2026, wakati akiwa mgeni rasmi katika Mahafali ya 20 ya Kidato cha Nne ya Shule ya Sekondari Kishapu, iliyopo Wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, ambapo amewapongeza walimu kwa juhudi zao za kuboresha ufaulu na kupunguza idadi ya wanafunzi wanaopata daraja sifuri.


Akizungumza katika mahafali hayo, Nangi amewataka wahitimu kuendelea kuwa na nidhamu wanapofanya mitihani na hata baada ya kumaliza shule, huku akiwahimiza kutoruhusu mazingira au watu wengine kuwakatisha tamaa katika kutimiza ndoto zao za elimu, bali wapambanie malengo yao kwa bidii na kujituma.


Aidha, amewataka wazazi na walezi kuendelea kuwafundisha watoto wao maadili mema, akisisitiza kuwa vijana ni hazina muhimu kwa familia, taifa na dunia kwa ujumla. Pia, amewapongeza walimu kwa jitihada za kuinua kiwango cha ufaulu na kuhakikisha wanafunzi wanapiga hatua kutoka daraja sifuri hadi madaraja ya ufaulu.


Katika risala yake kwa mgeni rasmi, Mkuu wa Shule ya Sekondari Kishapu, Mwalimu Buhoro Mipawa, amesema shule hiyo imepata mafanikio mbalimbali ikiwamo kuimarika kwa ufaulu wa wanafunzi, huku miundombinu ya madarasa ikiendelea kuboreshwa na kuwa katika hali inayokidhi mahitaji ya wanafunzi.


Hata hivyo, ameeleza changamoto zinazowakabili kuwa ni pamoja na uhaba wa vifaa vya michezo, hususan jezi na mipira, upungufu wa vifaa vya TEHAMA kutokana na ongezeko la wanafunzi, pamoja na kukosekana kwa mashine ya kudurufu mitihani na nyaraka nyingine za shule. Amesema upatikanaji wa mashine hiyo utasaidia kurahisisha shughuli za kitaaluma na kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji.


Kwa upande wao, wanafunzi wa Kidato cha Nne, kupitia risala iliyoandaliwa na wahitimu hao na kusomwa na Elizabeth Jacobo na Ebenezer Samweli, wameeleza mafanikio na changamoto za shule, huku wakibainisha kuwa wamepiga hatua katika ufaulu na kwamba madarasa yaliyoboreshwa yanatosheleza mahitaji yao. Hata hivyo, wameomba msaada wa vifaa vya michezo na vifaa vya TEHAMA ili kuimarisha zaidi shughuli za kitaaluma na michezo shuleni hapo.


Shule ya Sekondari Kishapu ilianzishwa mwaka 2004 ikiwa na wanafunzi 86, wavulana 43 na wasichana 43, pamoja na walimu watano. Kwa sasa, shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 862, wakiwamo wavulana 322 na wasichana 540, huku ikiwa na walimu 30, wanaume 20 na wanawake 10. Mahafali hayo ya 20 yamewahusisha wanafunzi 108 wa Kidato cha Nne, wavulana 49 na wasichana 59, ambao wanatarajiwa kuendeleza safari yao ya elimu na kuwa chachu ya maendeleo katika familia na taifa.
Makamo Afisa Elimu Sekondari Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Winfrida Mkama akizungumza kwenye Mahafali ya 20 ya Kidato cha Nne ya Shule ya Sekondari Kishapu yaliyofanyika Oktoba 9,2026
Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Sekondari Kishapu wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga Paul Makolo akizungumza kwenye Mahafali ya 20 ya Kidato cha Nne ya Shule ya Sekondari Kishapu yaliyofanyika Oktoba 9,2026
Mkuu wa Shule ya Sekondari Kishapu wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga, Mwalimu Buhoro Mipawa akisoma risala ya Shule mbele ya Mgeni rasmi wa Mahafali hayo ya 20 ya Shule hiyo Oktoba 9,2026
Wasoma risala ya wahitimu wa kidato cha nne mahafali ya 20 Shule ya Sekondari Kishapu iliyoko wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Elizabeth Jacobo(kulia) na Ebenezer Samweli(kushoto) Oktoba 9,2026








Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com