Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MKUTANO WA CATA UANGAZIE MIJADALA YA KUHAMASISHA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KATIKA UKUSANYAJI MAPATO - MAKAMU WA RAIS



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi amesema matumizi ya mifumo ya kisasa ya teknolojia ni chachu katika ukusanyaji wa kodi hivyo yanapaswa kutiliwa mkazo ili kuongeza uwazi, kuimarisha usimamizi wa kodi na kurahisisha ulipaji kodi.

Makamu wa Rais ameyasema hayo jijini Arusha Oktoba 06, 2026 wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa wa Chama cha Wasimamizi wa Kodi wa Jumuiya ya Madola (CATA) na kueleza kuwa teknolojia ni nyenzo muhimu katika kuboresha ukusanyaji wa mapato ya ndani na kuimarisha huduma kwa walipa kodi ndiyo maana mkutano huo umekuja na kauli mbiu inayogusa teknolojia.

Amesema pamoja na umuhimu wa teknolojia, mafanikio katika ukusanyaji wa mapato hayawezi kutegemea teknolojia pekee, bali yanahitaji sera nzuri, madhubuti, zinazoeleweka na zinazotabirika, pamoja na usimamizi wa kodi wenye ufanisi na unaokidhi mahitaji ya walipakodi.

Makamu wa Rais pia amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika masuala ya kodi, akibainisha kuwa biashara zinazovuka mipaka, makampuni ya kimataifa, miamala ya kidijitali pamoja na mali za kifedha zinazohifadhiwa nje ya nchi zimefanya ushirikiano kati ya mamlaka za kodi kuwa muhimu zaidi.

Amesema Tanzania inaendelea kuimarisha ushiriki wake katika ushirikiano wa kimataifa wa kodi, ikiwemo kubadilishana taarifa za kodi na kutoa msaada wa kiutawala baina ya nchi huku akieleza kuwa ushirikiano huo ni muhimu katika kuongeza uhakika wa kodi, kubadilishana taarifa, kuzuia na kutatua migogoro ya kikodi.

Amesema uratibu mzuri kati ya nchi unaweza kusaidia kulinda mapato ya Serikali huku ukipunguza uwezekano wa kutozwa kodi mara mbili na kuondoa sintofahamu kwa wawekezaji halali.

“Nchi inayovutia uwekezaji siyo ile isiyokuwa na kodi, bali ni ile yenye kanuni za kodi zilizo wazi, thabiti na zinazosimamiwa kwa haki, zikiungwa mkono na taratibu bora za forodha na ukusanyaji wa mapato,” amesema.

Awali akizungumza katika mkutano huo Rais wa CATA Mhe. Abu Tariq Jamaluddin amesema matumizi ya teknolojia ya kisasa yamekuwa yakisaidia nchi wanachama wa CATA kurahisisha utawala wa kodi kwa kuweka mazingira rahisi ya ukusanyaji wa mapato na kuwasaidia walipakodi kufuata sheria za kodi.

Amesema kauli mbiu ya mkutano huo inalenga kuhimiza matumizi zaidi ya teknolojia na kueleza kuwa CATA itaendelea kuwezesha matumizi ya teknolojia katika ukusanyaji wa kodi ili kuimarisha usimamizi wa kodi baina ya nchi wanachama.

Amesema kupitia mkutano huo nchi washiriki wataweza kubadilishana ujuzi na uzoefu kuhusu usimamizi wa kodi na matumizi ya teknolojia.

Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambao ndiyo waandaaji wa mkutano huo Bw. Yusuph Juma Mwenda amesema Mamlaka hiyo imepiga hatua kubwa katika matumizi ya teknolojia ambayo yameboresha zaidi huduma za usimamizi wa kodi kwa kuongeza uwazi na ufanisi.

Amesema kupitia matumizi ya teknolojia TRA imekuja na mfumo wa IDRAS unaosimamia kodi za ndani ambao unamuwezesha Mlipakodi kutoa risiti za kielektroniki kwa kutumia simu ya mkononi bila kuwa na mashine hali ambayo imeongeza uhiari katika kulipa kodi na kupunguza kuonana kwa walipakodi na maofisa wa TRA.

Amesema kupitia mkutano huo wataweza kubadilishana ujuzi na mataifa mengine akieleza kuwa matumizi ya teknolojia ya kisasa pia kwa Tanzania yameongeza wigo wa kodi kutokana na kuwapa uhuru walipakodi kujisajili kupitia mtandao na kupata namba ya utambulisho wa mlipakodi (TIN).

Mkutano huo utadumu mpaka Oktoba 09 mwaka huu.





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com