Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TARURA NJOMBE YAENDELEA KUBORESHA MIUNDOMBINU YA BARABARA

#Wananchi sasa kuzifikia huduma za kijamii kirahisi

Njombe

Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Wilaya ya Njombe imeendelea na kazi ya uboreshaji wa miundombinu ya barabara ili kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji kwa wananchi.

Hayo yamebainishwa na Meneja wa TARURA katika wilaya hiyo Mhandisi Costantine Ibengwe ambaye ameitaja miradi inayotekelezwa kwa sasa kuwa ni pamoja na ujenzi wa Barabara ya NBC- Kibena  kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita 2.84, mradi wa ujenzi wa daraja la mawe lenye urefu wa mita 31  linalounganisha Kata za Mji Mwema na Ramadhani ambapo ujenzi huo umefikia asilimia 70.

Kwa mujibu wa Mhandisi Ibengwe mradi mwingine unaotekelezwa katika Wilaya hiyo ni pamoja na ujenzi wa Barabara ya Mama White Kilomita 1.5 kwa kiwango cha changarawe ambapo  barabara hiyo tayari imekamilika na inatumika.

" TARURA katika Wilaya ya Njombe tunatekeleza miradi hii ili kuwawezesha wananchi kusafiri kwa urahisi na kufanya shughuli zao za kila siku bila shida" . Amefafanua Mhandisi Ibengwe.

Aidha, amesema kuwa ujenzi wa barabara ya Mama White umefanyika ili kuwezesha wananchi kufika kwa urahisi katika barabara kuu ya Songea pamoja na Ofisi za Mkuu wa Mkoa lakini pia kufika kwa urahisi katika Kituo cha Afya cha Mji mwema.

Kwa upande wake, Bw. Maulus Mlowe ambaye ni mkazi wa Njombe ameipongeza TARURA kwa kazi zinazoendelea na kusema kuwa miundombinu hiyo inawasaidia wananchi kuzifikia huduma za kijamii kwa urahisi.

" Zamani eneo hili lilikuwa halipitiki ila sasa imekua njia rahisi kwetu pia na wananfunzi wanapita kwa urahisi". Amesema Bw. Mlowe



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com