Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MKUTANO WA CATA 46 WATANGAZA UTALII KIMATAIFA


 
Baada ya kuhitimishwa kwa mkutano wa 46 wa Chama cha Wasimamizi wa Kodi wa Jumuiya ya Madola (CATA), Wajumbe kutoka Nchi 21 zikizoshiriki mkutano huo wametembelea Hifadhi ya Ngorongoro kujionea Vivutio vya utalii na Wanyamapori mbalimbali wanaopatikana Nchini Tanzania.

Ziara hiyo imefanyika ikiwa ni sehemu ya shughuli zilizofuatia mkutano huku Washiriki wakipata nafasi ya kutembelea hifadhi hiyo na kujionea uzuri wa mazingira ya asili ya Tanzania.

Akizungumza kuhusu ziara hiyo kwa niaba ya Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Juma Mwenda,  Kamishna wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa Bw. Juma Hassan, amesema lengo ni kuwapa wajumbe fursa ya kuona Vivutio vya Utalii vilivyopo Nchini ili waweze kuvitangaza katika Nchi zao na kuhamasisha Watalii zaidi kuitembelea Tanzania jambo ambalo litaongeza mapato ya nchi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa CATA, Esther Koisin, ameishukuru TRA kwa kuwawezesha kutembelea Ngorongoro, akisema ziara hiyo imewapa nafasi ya kuona wanyamapori wakiishi katika mazingira yao ya asili na kusifia uzuri wa nchi ya Tanzania

Hata hivyo, mmoja wa Washiriki kutoka Malaysia, Baharuddin, amesema amevutiwa na wanyama mbalimbali aliowaona, wakiwemo Tembo, Kiboko, Swala, Twiga, Kifaru, Fisi, Pundamilia na ndege wa aina mbalimbali pamoja na ukarimu wa Watanzania.

Ziara hiyo inatarajiwa kusaidia kuitangaza Tanzania kimataifa na kuongeza hamasa ya Wageni wengine kutembelea Vivutio vya utalii Nchini.





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com