
Katika ziara hiyo iliyofanyika Oktoba 20,2026, Kamanda Magomi amesisitiza umuhimu wa wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kudumisha amani na usalama katika maeneo yao.
Aidha, ameeleza kuwa dhamana haitolewi kwa malipo ya fedha, bali kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa, huku akiwahimiza wananchi kufahamu haki zao na kutoa taarifa kwa vyombo vya dola wanapokutana na changamoto za kiusalama.
Sambamba na hilo, amewahimiza wanaume kutokuwa na hofu ya kuripoti matukio ya ukatili wanayofanyiwa, akisisitiza kuwa ukatili hauna budi kuripotiwa ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa mujibu wa sheria.
Amesema ushiriki wa kila mwananchi ni muhimu katika kukabiliana na vitendo vya ukatili na kujenga jamii salama.
Kuhusu usalimishaji wa silaha haramu, Kamanda Magomi amewahimiza wananchi wenye silaha hizo kuzisalimisha kabla ya Oktoba 31, 2026, ambayo ndiyo mwisho wa kampeni hiyo.
Ameeleza kuwa baada ya muda huo kupita, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika kumiliki silaha haramu, hivyo kuwataka wananchi kutumia muda uliobaki kutekeleza agizo hilo.
Katika mikutano hiyo, wananchi pia waliwasilisha changamoto zinazowakabili, ikiwemo ugumu wa madereva wa bajaji kupata leseni za udereva na uhitaji wa makoti ya mvua kwa askari wa Sungusungu wa Wendele kuelekea msimu wa masika.
Kuhusu changamoto hizo, OCD wa Kahama ameahidi kutoa makoti 10 ya mvua kwa Sungusungu wa Wendele, huku DTO na OCD wa Kahama wakitarajiwa kuzungumza na vyuo vya udereva ili kuwezesha madereva kupata mafunzo na vyeti vinavyohitajika kwa gharama nafuu ili kukidhi masharti ya kupata leseni.





TAFUTA HABARI
Kamusi
Social Plugin