Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

JESHI LA POLISI LATOA ONYO KWA WAMILIKI WA SILAHA HARAMU, MUDA WA MSAMAHA KUSALIMISHA KUMALIZIKA OKTOBA 31



Jeshi la Polisi Tanzania limewaonya wananchi wanaomiliki silaha kinyume cha sheria kuzitumia fursa ya msamaha wa kusalimisha silaha hizo kabla ya muda wa msamaha kumalizika Oktoba 31, 2026, likisisitiza kuwa kuanzia Novemba Mosi, mwaka huu, litaanza misako nchi nzima na kuwachukulia hatua za kisheria wote watakaobainika kumiliki silaha haramu.

Kampeni hiyo ilizinduliwa Agosti 31, 2026, na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Paschal Katambi, jijini Dodoma, ikilenga kupunguza vitendo vya uhalifu na kuimarisha usalama wa wananchi.

Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi iliyotolewa Oktoba 20, 2026, kuanzia Septemba Mosi hadi Oktoba 19, mwaka huu, jumla ya silaha 230 zilisalimishwa, zikiwemo AK 47 tano, rifle 15, shotgun 50, bastola nane, Mk IV mbili na magobore 150. Jeshi hilo limeeleza kuwa silaha hizo zimesalimishwa katika kipindi cha kampeni inayotoa fursa kwa wananchi wanaomiliki silaha kinyume cha sheria kuzikabidhi kwa mamlaka husika bila kuchukuliwa hatua za kisheria, kwa mujibu wa masharti ya msamaha huo.

Jeshi la Polisi limewataka wananchi wenye silaha hizo kuzisalimisha katika vituo vya polisi, ofisi za Serikali za mitaa au vijiji na ofisi za watendaji wa kata au shehia, kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa kumi jioni.

Silaha zinazolengwa ni pamoja na bastola, shotgun, rifle, magobore na silaha nyingine zinazomilikiwa bila vibali halali au ambazo hazijawahi kusajiliwa nchini.

Aidha, wananchi wanaomiliki silaha kihalali lakini kwa sasa wanakabiliwa na changamoto za kiafya, uzee au sababu nyingine zinazowafanya washindwe kuzitunza wanahimizwa kuzisalimisha ili kuzuia madhara yanayoweza kujitokeza kwa familia na jamii.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com