Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DC NYANGASA AMPONGEZA RAIS DKT.SAMIA UWEKEZAJI BANDARI YA TANGA

 

Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa imepanga kutumia fursa za uwekezaji zinazopatikana katika Bandari ya Tanga, ikiwemo ujenzi wa Bandari Kavu na Gati jipya litakaloongeza uwezo wa bandari hiyo kuhudumia meli na mizigo zaidi.

Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Fatma Nyangasa, ameongoza ujumbe wa Halmashauri hiyo kutembelea Bandari ya Tanga kwa lengo la kujifunza na kuona namna uwekezaji wa Shilingi Bilioni 430 ulivyotekelezwa katika bandari hiyo.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Fatma Nyangasa amesema, “Wasimamizi wa Bandari ndio wanaowezesha dhima ya Mheshimiwa Rais iweze kutekelezeka, ndani ya miaka minne imewekeza kiasi cha Shilingi Bilioni 430, sio hela ndogo.”


Aidha amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka msisitizo katika uwekezaji na maendeleo ya miundombinu ya bandari, akisema hatua hiyo imeendelea kuleta mabadiliko makubwa katika shughuli za kiuchumi na kuongeza fursa kwa wananchi.

Ameongeza kuwa wanakwenda kujipanga kuhakikisha wanatumia yale waliyoyaona katika maendeleo na waliyojifunza ili kupata matokeo mazuri na Halmashauri ya Kondoa iweze kunufaika na fursa zinazopatikana.

Kwa upande wake, Meneja wa Bandari ya Tanga, Salehe Mbega, amesema wamefanya tathmini na kugundua kuwa ni vema kushirikisha sekta mbalimbali kuja kuwekeza katika shughuli za bandari.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania, inahitajika zaidi ya Shilingi Trilioni 11 kwa ajili ya uwekezaji katika maeneo mbalimbali ya bandari nchini, hali inayowafanya kuwashirikisha wadau na wawekezaji katika kuchangia maendeleo ya sekta hiyo.

Baadhi ya viongozi walioambatana na msafara huo katika Bandari ya Tanga, akiwemo Diwani wa Kondoa, Said Ndwata, amesema ameshangazwa na namna bandari hiyo inavyofanya kazi kutokana na maboresho yaliyofanyika.

Said Ndwata amesema ndani ya miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kumekuwa na maboresho makubwa katika bandari hiyo, hali iliyosaidia kuongeza kiwango cha mizigo inayohudumiwa, huku sehemu ya mizigo hiyo ikienda katika nchi za jirani.

Naye Katibu wa Mwenezi wa CCM Wilaya ya Kondoa, Kimolo Darabu, amesema kuboreshwa kwa Bandari ya Tanga kumeongeza fursa za ajira kwa wakazi wa Tanga na maeneo mengine nje ya mkoa huo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com