Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WCF YAWEKA MKAZO ULINZI WA WAFANYAKAZI SEKTA YA MADINI WAZIRI SANGU



Na Sheila Ahmadi, Geita

Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) umeendelea kuweka mkazo katika kuhakikisha wafanyakazi, hususan wanaofanya kazi katika sekta zenye mazingira hatarishi kama madini, wanalindwa na kupata stahiki zao pale wanapopatwa na madhara yatokanayo na kazi.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, amesema waajiri wana wajibu wa kuhakikisha wafanyakazi wao wanakuwa ndani ya mfumo wa WCF kwa kuwasajili na kuwasilisha michango kwa wakati.

Sangu ameyasema hayo Septemba 24, 2026, baada ya kutembelea banda la WCF katika Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, mkoani Geita.

Amesema uzingatiaji wa taratibu za WCF ni muhimu zaidi katika sekta ya madini kutokana na mazingira ya kazi yanayoweza kuwa na changamoto za kiusalama na kiafya kwa wafanyakazi.

Waziri Sangu Amesema kuwa waajiri wanapotekeleza wajibu wao kwa kuwasilisha michango kwa wakati, huweka mazingira bora ya kuwawezesha wafanyakazi na wategemezi wao kupata stahiki pale mfanyakazi anapopatwa na ajali au madhara yanayostahili fidia kwa mujibu wa sheria.

Katika ziara hiyo, Waziri Sangu pia alielezwa kuhusu hatua zinazochukuliwa na WCF kutoa elimu kwa waajiri na wafanyakazi kuhusu haki zao, wajibu wa waajiri pamoja na taratibu za kupata fidia.

Naye Mkurugenzi wa WCF, Dkt. John Mduma, amesema taasisi hiyo imeendelea kutumia teknolojia za kidigitali kurahisisha huduma kwa waajiri na wafanyakazi.

Amesema mifumo hiyo inawawezesha waajiri kufanya usajili na kuwasilisha malipo kwa njia ya mtandao bila kulazimika kufika katika ofisi za WCF.

Mduma amesema WCF pia imeendelea kutumia teknolojia za simu kusogeza huduma karibu na wananchi, huku ikitumia maonesho ya madini kuwaelimisha wadau kuhusu huduma zinazotolewa, wajibu wa waajiri na haki za wafanyakazi.

hatua hizo ni sehemu ya juhudi za taasisi hiyo kuhakikisha taarifa kuhusu fidia na taratibu za WCF zinawafikia wadau kwa urahisi, hususan katika sekta ya madini yenye idadi kubwa ya wafanyakazi wanaokabiliwa na mazingira mbalimbali ya kazi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com