Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KIJANI KONSET YAWALETEA WAKULIMA GEITA FURSA YA MBEGU BORA




Na Sheila Ahmadi, Geita


WAKULIMA mkoani Geita wamepatiwa fursa ya kupata mbegu bora za kilimo pamoja na elimu ya matumizi sahihi ya mbegu hizo kupitia Taasisi ya Kijani Konset inayoshiriki katika Maonesho ya Madini yanayoendelea mkoani humo.

Fursa hiyo inalenga kuwasaidia wakulima kuongeza uzalishaji na tija katika kilimo kwa kutumia mbegu zilizothibitishwa na zinazokidhi mahitaji ya kilimo cha kisasa.

Akizungumza katika maonesho hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kijani Konset, Mandolin Kahindi, amesema taasisi hiyo imejikita katika kuwaunganisha wananchi na fursa zinazopatikana katika sekta mbalimbali, ikiwemo kilimo, uhifadhi wa mazingira, maliasili na utalii.

Amesema kupitia ushirikiano na Wakala wa Mbegu za Kilimo Tanzania (ASA), Kijani Konset inawafikishia wakulima mbegu mbalimbali zilizothibitishwa, zikiwemo za mahindi, mpunga na mbogamboga.

“Tunataka kuhakikisha wakulima wanapata mbegu bora, lakini pia wanapata elimu ya namna ya kuzitumia ili waweze kuongeza uzalishaji na kupata mavuno yenye tija,” amesema Kahindi.


Kwa mujibu wa taasisi hiyo, baadhi ya mbegu zinazotolewa zina uwezo wa kustahimili changamoto za ukame, magonjwa na wadudu, hali inayoweza kuwasaidia wakulima kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika uzalishaji wa mazao.

Kwa upande wake, Afisa Kilimo wa Kijani Konset, Matilda Philipo, amesema taasisi hiyo haitoi mbegu pekee, bali pia inawapatia wakulima elimu kuhusu matumizi sahihi ya mbegu na kanuni bora za kilimo.

elimu hiyo ni muhimu kwa kuwa upatikanaji wa mbegu bora pekee hautoshi bila mkulima kuwa na uelewa wa namna ya kuzitumia, kuzitunza na kuzingatia kanuni za kilimo ili kupata mavuno yanayotarajiwa.

Katika kuwekeza katika kilimo bora kuna umuhimu mkubwa katika kuongeza kipato cha wakulima, kuimarisha uzalishaji wa chakula na kusaidia jamii zinazojihusisha na shughuli mbalimbali za kiuchumi, ikiwemo uchimbaji wa madini.

Kijani Konset imewahimiza wakulima na wananchi wanaotembelea maonesho hayo kufika katika banda lake lililopo ndani ya banda kubwa la Halmashauri ya Wilaya ya Geita, ili kupata taarifa kuhusu mbegu bora na elimu ya kilimo.

Hatua hiyo inatajwa kuwa sehemu ya juhudi za kuwawezesha wakulima kutumia teknolojia na pembejeo bora katika kuongeza uzalishaji, kipato na usalama wa chakula












.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com