Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WATU 25 MBARONI KWA TUHUMA ZA MAUAJI,VURUGU ZA WAKULIMA NA WAFUGAJI TUNDURU

moja ya Ofisi ya Serikali iliyochomwa moto katika mgogoro wa wafugaji na wakulima kijiji cha Mbesa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma SACP Marco G Chilya akizungumza kuhususiana na vurugu na mauaji yaliyotokea kwa nyakati tofauti kati ya wakulima na wafugaji wilayani Tunduru 

Na Regina Ndumbaro, Tunduru-Ruvuma

Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma linawashikilia watu 25 wanaodaiwa kuhusika na mfululizo wa matukio ya mauaji na vurugu yanayodaiwa kuchochewa na migogoro kati ya wakulima na wafugaji wilayani Tunduru, ambapo watu watatu wameuawa na wengine wawili kujeruhiwa. 

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Marco G. Chilya, amesema kati ya watuhumiwa hao, wanane wanahusishwa na matukio ya mauaji huku 17 wakihusishwa na vurugu, wakiwemo wafugaji 10 na wakulima 15.

 Kamanda Chilya ametoa taarifa hiyo baada ya kufika katika maeneo yaliyoathiriwa na kujionea uharibifu wa mali, ikiwemo kuchomwa kwa Ofisi za Serikali na kuharibiwa kwa gari la Polisi, huku akisema operesheni na upelelezi vinaendelea kuwabaini na kuwakamata wahusika wengine.

Mfululizo wa matukio hayo ulianza Septemba 17, 2026, katika Kijiji cha Mrusha, Tarafa ya Lukumbule, baada ya mfugaji Shimbi Upole Shimbi, miaka 45, kutoa taarifa kuwa ng’ombe wake 180 waliporwa na kundi la wananchi wanaodaiwa kuwa wakulima na kuondoka nao kuelekea Kijiji cha Chikomo. 

Mfugaji huyo akiwa na ndugu zake alianza kuwatafuta ng’ombe hao na kufanikiwa kuwapata 179 katika pori la Kijiji cha Chinunje, Kata ya Mbesa, Tarafa ya Nalasi, huku ng’ombe mmoja pamoja na mchungaji Msanja Shimbi Upule wakiwa hawajaonekana.

Septemba 18, 2026, wafugaji walimtafuta mchungaji huyo na kumkuta ameuawa, mwili wake ukiwa umezamishwa kwenye matope katika Mto Chermambo, Kijiji cha Chinunje. 

Baada ya tukio hilo, wafugaji walivamia Vijiji vya Chikomo na Chinunje, ambapo Mohamed Kasim Chabwela, miaka 58, aliuawa, huku Yusuph Yasin Bakili, miaka 42, na Rashid Ally Ahmad, miaka 49, wakijeruhiwa. Hata hivyo, Septemba 21, 2026, hali ilizidi kuwa tete baada ya wanakijiji wa Mbesa kupata taarifa kuwa mkulima mwenzao aliyekuwa akiishi mashambani ameuawa na kitu chenye ncha kali. 

Kikao cha wanakijiji kilichoitishwa kujadili tukio hilo kilivunjika bila mwafaka na baadaye kuzuka vurugu zilizoshuhudia kuchomwa kwa Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Mbesa, Ofisi ya Kijiji cha Airport Mbesa na nyumba ya Serikali aliyokuwa akiishi Afisa Kilimo na Mifugo.

Katika vurugu hizo, mali nyingine za Serikali ziliharibiwa, ikiwemo jembe la trekta, huku gari la Polisi likivunjwa kioo. 

Jeshi la Polisi limewataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi, kupora au kuchinja mifugo na pia kuacha kuingiza mifugo katika mashamba na kuharibu mazao, likisisitiza kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika kuhusika na matukio hayo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com