Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

VIONGOZI 30 WACHAGULIWA KUONGOZA BURUNGE WMA


Viongozi wapya wa Burunge WMA kutoka Kijiji cha Olasiti, Wilaya ya Babati, Mkoa wa Manyara, waliochaguliwa kuongoza na kusimamia masuala ya uhifadhi na maendeleo ya jamii.
Wananchi wa Burunge wakipiga kura katika uchaguzi wa viongozi wa Burunge WMA.
Wananchi wa Kijiji cha Olasiti wakishiriki katika uchaguzi wa viongozi wa Burunge WMA, Wilaya ya Babati, Mkoa wa Manyara.
Wananchi wa Burunge wakipiga kura katika uchaguzi wa viongozi wa Burunge WMA.
Diwani wa Kata ya Ngaiti, Stevin Mollel, akizungumza wakati wa uchaguzi wa viongozi wa Burunge WMA, Wilaya ya Babati, Mkoa wa Manyara.

Na Mwandishi Wetu, BABATI

Halmashauri ya Wilaya ya Babati Vijijini, Mkoa wa Manyara, imekamilisha uchaguzi wa viongozi 30 watakaounda uongozi wa Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Burunge (Burunge Wildlife Management Area – WMA), baada ya viongozi waliokuwepo kumaliza muda wao wa uongozi.

Viongozi hao wamechaguliwa kutoka katika vijiji 10 vinavyounda Burunge WMA, ambapo kila kijiji kimechagua wajumbe watatu watakaowakilisha kijiji chao katika uongozi wa jumuiya hiyo.

Akizungumza jana wakati wa kuhitimisha uchaguzi katika Kijiji cha Olasiti, kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati Vijijini, Afisa Wanyamapori wa Wilaya ya Babati, Christopher Laizer, amesema uchaguzi huo umefanyika baada ya viongozi waliokuwepo kumaliza muda wao wa uongozi.

Laizer amesema kabla ya kumalizika kwa muda wao wa uongozi mwezi Juni mwaka huu, viongozi hao walikuwa wamesimamishwa kwa muda ili kupisha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali zilizokuwa zikihusishwa na uendeshaji wa jumuiya hiyo.

“Kwa mujibu wa Sheria ya Wanyamapori, Mkurugenzi wa Halmashauri ndiye mwenye wajibu wa kuitisha na kusimamia uchaguzi, jambo ambalo limekamilika,” amesema Laizer.

Katika uchaguzi uliofanyika katika Kijiji cha Olasiti, viongozi watatu waliochaguliwa ni Ngotei Lomayani, aliyepata kura 153, Fred Saitabau aliyepata kura 84 na Loseku Sanin’go, aliyepata kura 169, baada ya kuwashinda wagombea wengine 10 waliojitokeza kugombea nafasi hizo.

WATAKA KUONGEZA MAPATO, KUPUNGUZA MIGOGORO

Baada ya kuchaguliwa, viongozi hao wameahidi kushirikiana na Serikali pamoja na wadau mbalimbali kuhakikisha Burunge WMA inaendelea kuimarika katika uhifadhi, kuongeza manufaa kwa wananchi na kuchangia maendeleo ya maeneo yanayolizunguka.

Lomayani amesema miongoni mwa vipaumbele vyao vitakuwa kuongeza mapato ya jumuiya hiyo na kushughulikia changamoto za migogoro kati ya wananchi na wanyamapori.

Amesema ushirikiano kati ya uongozi wa Burunge WMA, Serikali na wananchi ni muhimu katika kuhakikisha shughuli za uhifadhi zinaendelea sambamba na wananchi kunufaika na rasilimali zilizopo katika eneo hilo.

Baada ya kukamilika kwa uchaguzi huo, wajumbe waliochaguliwa kutoka katika vijiji 10, maarufu kama AA, wanatarajiwa kumchagua Mwenyekiti wa Jumuiya ya Burunge WMA pamoja na kuchagua Bodi itakayokuwa na jukumu la kusimamia shughuli za jumuiya hiyo.

VIONGOZI WAPYA WATAKIWA KUIJENGA BURUNGE WMA

Diwani wa Kata ya Ngaiti, Stevin Mollel, amewataka viongozi wapya kutumia nafasi waliyopewa kuhakikisha Burunge WMA inakuwa miongoni mwa maeneo bora ya uhifadhi barani Afrika.

Mollel amesema kwa sasa mapato ya Burunge WMA yamefikia takribani Shilingi bilioni nne kwa mwaka, hivyo uongozi mpya unapaswa kuweka mikakati ya kuongeza mapato hayo na kuhakikisha manufaa yake yanaonekana kwa wananchi.


“Tunawataka wasirudie kuleta migogoro ambayo ilisababisha kusimamishwa kwa viongozi wote waliopita. Tuna imani kubwa sasa kwa sababu viongozi wengi waliochaguliwa ni sura mpya,” amesema Mollel.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati Vijijini, Anna Mbogo, amesema uchaguzi huo umefanyika baada ya kukamilika kwa maboresho ya Katiba pamoja na mfumo wa uendeshaji wa Burunge WMA.

Amesema maboresho hayo yamelenga kuimarisha utawala na uendeshaji wa jumuiya hiyo, pamoja na kuweka mazingira bora ya usimamizi wa shughuli za uhifadhi na maendeleo ya jamii.

Burunge WMA ni eneo la uhifadhi linalopatikana kati ya Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara, jambo linalolifanya kuwa eneo muhimu katika mfumo wa kiikolojia na uhifadhi wa wanyamapori nchini Tanzania.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com