Na Mwandishi Wetu , Dar es Salaam
Maboresho yanayoendelea katika Bandari ya Dar es Salaam yameanza kuongeza ufanisi wa utoaji huduma, kuvutia meli zaidi na kuchochea ongezeko la shehena pamoja na mapato yanayotokana na shughuli za bandari hiyo.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Prof. Godius Kahyarara, wakati akizungumza na wadau mbalimbali wa sekta ya usafirishaji na bandari katika kikao cha maboresho ya Bandari (PIC) kilichofanyika katika ukumbi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), jijini Dar es Salaam.
Prof. Kahyarara amesema uwepo wa vifaa vya kisasa na kuimarika kwa kasi ya kuhudumia meli ni miongoni mwa sababu zinazochangia kuongezeka kwa idadi ya meli zinazoingia katika Bandari ya Dar es Salaam.
Aidha hali hiyo inahitaji ushirikiano zaidi miongoni mwa wadau wa sekta hiyo ili kuhakikisha shehena inayoshushwa bandarini inatolewa kwa wakati na hivyo kuongeza ufanisi wa mnyororo mzima wa usafirishaji.
“Kutokana na uwepo wa vifaa vya kisasa na meli kuhudumiwa kwa wakati, hii imeongeza kuvutia meli kuongezeka katika Bandari ya Dar es Salaam. Hivyo, wadau tuendelee kushirikiana kwa kutoa mizigo kwa wakati,” amesema Prof. Kahyarara.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI anayeshughulikia Miundombinu, Rogatus Mativila, amesema Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) inaendelea kuhakikisha barabara za mitaa, hususan zinazounganisha maeneo ya bandari kavu, zinapitika kwa ajili ya kurahisisha usafirishaji wa shehena.
Mativila amesema uboreshaji wa miundombinu ya barabara ni sehemu muhimu ya kuhakikisha ongezeko la shehena bandarini linaendana na uwezo wa kusafirisha mizigo kutoka bandarini kwenda maeneo mbalimbali kwa ufanisi.
Naye Meneja Uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam, Frank Korasa, amesema kiwango cha shehena kinachopitia bandarini hapo kimeongezeka kwa kiasi kikubwa, huku shehena hiyo ikijumuisha magari, makaa na mizigo ya aina mbalimbali.
Katika Hatua nyingine Kampuni ya DP World imesema inaendelea kuwekeza katika ununuzi wa mitambo ya kisasa kwa ajili ya kuongeza ufanisi wa kuhudumia meli na shehena katika Bandari ya Dar es Salaam.
Vilevile Kampuni hiyo imeongeza kuwa inaendelea kufanya maboresho katika maeneo ya kuhifadhia shehena, ikiwemo kuhakikisha mizigo inalindwa dhidi ya changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa msimu wa mvua.
Sanjari na Hayo kikao hicho kimehusisha wadau mbalimbali, wakiwemo TPA, TRA, wamiliki wa malori, Wizara ya Ulinzi, Wizara ya Uchukuzi, pamoja na wamiliki wa bandari kavu, kwa lengo la kujadili namna ya kuongeza ufanisi katika utoaji na usafirishaji wa shehena kutoka bandarini.






Social Plugin