Na Mwandishi Wetu, MEATU
Taasisi ya uhifadhi ya Friedkin Conservation Fund (FCF) kwa kushirikiana na kampuni ya uhifadhi na utalii ya Mwiba Holdings Ltd (MHL) imetoa baiskeli 400 kwa wanafunzi wa shule za sekondari katika Wilaya ya Meatu, Mkoa wa Simiyu, kwa lengo la kuwawezesha kufika shuleni kwa wakati na kupunguza changamoto ya usafiri wanayokabiliana nayo.
Baiskeli hizo zimetolewa kwa wanafunzi kutoka vijiji vya Ming’ongwa, Butuli, Bulyandulu na Mwangudo, wanaosoma katika shule za sekondari za Busangwa, Paji na Mwangudo.
Akitoa taarifa kuhusu miradi ya maendeleo inayotekelezwa na FCF na Mwiba Holdings katika Wilaya ya Meatu, Afisa Miradi wa Kitengo cha Ufugaji Nyuki wa Friedkin, Baraka Mabula, amesema mradi huo wa baiskeli ulianza mwaka 2023 na unaendelea hadi sasa.
Mabula amesema jumla ya wanafunzi 400 wamenufaika na mpango huo, wakiwemo wavulana 188 na wasichana 212, huku baiskeli hizo zikiendelea kufanyiwa ukarabati mara kwa mara ili kuhakikisha zinakuwa katika hali nzuri na zinaendelea kutumika kwa muda mrefu.
Amesema mradi huo unalenga zaidi kuwasaidia wanafunzi wanaoishi katika maeneo yaliyo mbali na shule, ikiwemo maeneo yanayozungukwa na wanyamapori, ambapo changamoto ya usafiri inaweza kuwa kikwazo kwa wanafunzi kufika shuleni kwa wakati.
“Mradi huu unawasaidia wanafunzi, hasa wale wanaoishi mbali na shule na katika maeneo yenye wanyamapori. Pia una lengo la kuinua viwango vya ufaulu katika Wilaya ya Meatu,” amesema Mabula.
Amesema utaratibu uliowekwa ni kwamba wanafunzi wanapotimiza masomo yao ya Kidato cha Nne wanatakiwa kuzirudisha baiskeli hizo shuleni, ambapo hutolewa kwa wanafunzi wengine wanaohitaji msaada huo.
UFADHILI WA MASOMO
Mbali na mradi wa baiskeli, Mabula amesema Friedkin Conservation Fund imekuwa ikiendesha pia mpango wa Friedkin Scholarship Award, unaolenga kuwasaidia wanafunzi kupata elimu katika ngazi mbalimbali.
Amesema ufadhili huo unawahusisha wanafunzi wanaojiunga na vyuo vikuu, vyuo vya kati pamoja na Kidato cha Tano na Sita (A-Level).
Kwa mujibu wa Mabula, hadi kufikia mwaka 2026, jumla ya wanafunzi 82, wakiwemo wavulana 50 na wasichana 32, wamepata ufadhili huo katika ngazi mbalimbali za elimu.
HALMASHAURI YAPONGEZA
Akizungumzia miradi hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Protas Dibogo, ameipongeza Friedkin Conservation Fund na Mwiba Holdings kwa mchango wao katika kuboresha elimu na kuunga mkono maendeleo ya jamii.
Dibogo amesema Halmashauri ya Meatu itaendelea kushirikiana na wawekezaji pamoja na asasi za kiraia zinazotekeleza miradi ya maendeleo katika wilaya hiyo.
“Halmashauri ya Meatu tutaendelea kuwaunga mkono wawekezaji wetu na asasi za kiraia zote ili mtimize malengo yenu,” amesema Dibogo.
Naye Mbunge wa Jimbo la Kisesa, Musa Godfrey Mbuga, amepongeza FCF na Mwiba Holdings kwa miradi hiyo, huku akiomba mipango hiyo ya kusaidia jamii, hususan katika sekta ya elimu, iendelee kupanuliwa ili kuwafikia wanafunzi wengi zaidi.
UWEKEZAJI WA MWIBA MEATU
Mwiba Holdings Ltd ilianza uwekezaji wake wa utalii katika Pori Tengefu la Makao Mwiba baada ya kuanzishwa mwaka 2008, huku kampuni hiyo ikiendelea kushiriki katika shughuli za uhifadhi na utalii.
Kuanzia Januari 2024, Mwiba Holdings ilipanua shughuli zake katika Pori la Akiba la Maswa baada ya kupata mkataba wa miaka 20 kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kwa ajili ya kufanya shughuli za biashara ya utalii.
Friedkin Conservation Fund (FCF) ni taasisi inayotekeleza shughuli mbalimbali za kijamii kwa niaba ya Mwiba Holdings katika jamii zinazozunguka Pori la Akiba la Maswa, ikiwemo kusaidia sekta ya elimu na miradi mingine ya maendeleo ya jamii.

Social Plugin