Dodoma
Ujenzi wa Miundombinu katika Mradi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato umefikia asilimia 89.02, huku kazi za ujenzi wa njia ya kurukia na kutua ndege, njia za viungio (taxiways) pamoja na eneo la maegesho ya ndege (apron) zikifikia zaidi ya asilimia 98.
Hayo yameelezwa leo, Septemba 24, 2026, na Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maendeleo ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato jijini Dodoma.
Mhandisi Besta amesema kuwa sehemu ya kwanza ya ujenzi wa miundombinu, ujenzi wa njia ya kurukia na kutua ndege umefikia asilimia 98, njia za viungio (taxiways) asilimia 99, huku eneo la maegesho ya ndege (apron) likiwa limefikia asilimia 99.
Aidha, amesema ujenzi wa barabara ya kuingia uwanjani, barabara za ndani na maegesho ya magari umefikia asilimia 75, mfumo wa maji asilimia 89, uzio na mageti asilimia 76, pamoja na kazi za umeme na vifaa vya kuongozea ndege kufikia asilimia 90.
Kwa mujibu wa Mhandisi Besta, kazi zilizobaki katika sehemu ya kwanza ni pamoja na upandaji wa nyasi katika maeneo ya usalama ya njia ya kurukia na njia za viungio (runway and taxiway strips), ufungaji wa taa za kuongozea ndege ardhini na taa za barabarani, mabomba na tanki la maji la chini ya ardhi, kukamilisha uzio na mageti, pamoja na ufungaji wa vifaa vya mawasiliano vya uongozaji wa ndege ikiwemo ILS na DVOR.
Ameeleza kuwa vifaa vya ILS na DVOR tayari vimewasili katika eneo la mradi, hivyo kinachofanyika ni kukamilisha taratibu za ufungaji na uunganishaji wa mifumo hiyo.
Katika hatua nyingine, Mhandisi Besta amesema sehemu ya pili inayohusisha ujenzi wa majengo imefikia asilimia 78.37, ambapo Jengo la Abiria limefikia asilimia 81, Mnara wa Kuongozea Ndege (Control Tower) asilimia 74, Kituo cha Huduma za Zimamoto asilimia 88, kituo kikubwa na vituo vidogo vya umeme asilimia 71, huku jengo la huduma za Hali ya Hewa (MTO) likifikia asilimia 87.
Amesema kazi zinazoendelea katika Package 2 ni pamoja na umaliziaji wa majengo, usimikaji wa mifumo ya mitambo ya uendeshaji wa uwanja, mifumo ya umeme na mabomba, ufungaji wa vifaa vya TEHAMA na mifumo ya mawasiliano, mashine za ukaguzi wa mizigo, umaliziaji wa madaraja ya kupitia abiria (Passenger Boarding Bridges), vifaa vya hali ya hewa pamoja na magari ya zimamoto.
Mhandisi Besta amesema ujenzi wa miundombinu unatarajiwa kukamilika ifikapo Novemba 27, 2026, huku ujenzi wa majengo ukitarajiwa kukamilika ifikapo Desemba 30, 2026.
Kukamilika kwa mradi huo kunatarajiwa kuongeza fursa za usafiri wa anga kwa wakazi wa Dodoma na maeneo mengine, kurahisisha usafiri kwa wasafiri wanaoingia na kutoka jijini Dodoma, pamoja na kuchochea shughuli za biashara na uwekezaji.




Social Plugin