
Afisa Usajili wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Minihajj Renard Mbegha (DRO) (kulia- aliyevaa suti) akimkabidhi mwananchi wa Kata ya Mwadui Lohumbo Emily Lusihila Kalimanzira(kushoto) kitambulisho chake cha NIDA wakati wa kuadhimisha Siku ya Utambulisho Duniani, iliyoadhimishwa Septemba 16, huku kiwilaya zikifanyika ofisi za Mamlaka hiyo iliyoko jengo la ofisi ya Mkuu wa Wilaya


Ofisi ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Wilaya ya Kishapu, mkoani Shinyanga, imeungana na ofisi nyingine za NIDA nchini pamoja na wananchi katika kuadhimisha Siku ya Utambulisho Duniani, inayoadhimishwa kila mwaka Septemba 16.
Maadhimisho hayo yamefanyika kwa lengo la kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa kuwa na utambulisho rasmi, pamoja na kuwafikishia elimu kuhusu huduma zinazotolewa na NIDA katika usajili na utambuzi wa watu.
Katika kuadhimisha siku hiyo, Ofisi ya NIDA Wilaya ya Kishapu imetoa huduma mbalimbali kwa wananchi, ikiwemo kugawa Vitambulisho vya Taifa kwa wananchi waliokamilisha taratibu za usajili, pamoja na kutoa elimu kuhusu usajili na utambuzi.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Wilaya ya Kishapu, Fatma Mohamed, amesema utambulisho rasmi ni muhimu kwa kila mwananchi kwa kuwa unamwezesha kutambulika kisheria na kurahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Fatma amesema Serikali kupitia NIDA imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wananchi kupata Vitambulisho vya Taifa, hivyo amewataka wananchi kutumia fursa hiyo kwa kuhakikisha wanakamilisha taratibu za usajili na kuchukua vitambulisho vyao pindi vinapokuwa tayari.
“Utambulisho ni jambo muhimu sana kwa kila mwananchi. Tunawahimiza wananchi wa Kishapu kuhakikisha wanasajiliwa na wanapata Vitambulisho vya Taifa, kwa sababu kitambulisho kinasaidia katika kupata huduma mbalimbali na pia kinamwezesha mwananchi kutambulika rasmi,” amesema Fatma.
Wananchi waliofika kwenye ofisi hizo wameeleza kufurahishwa na huduma hizo, wakisema elimu waliyoipata imewasaidia kuelewa zaidi umuhimu wa kuwa na Kitambulisho cha Taifa na namna ya kutumia huduma za NIDA.
Mkazi wa Kata ya Mwadui Emily Lusihila Kalimanzira, amesema maadhimisho hayo yamempa fursa ya kupata elimu kuhusu umuhimu wa kuwa na Kitambulisho cha Taifa, huku akiwahimiza wananchi wengine kuhakikisha wanakuwa na utambulisho rasmi.

Afisa Usajili Mwandamizi Fred Anyagile Mwasipu akizungumza wakati wa kuadhimisha Siku ya Utambulisho Duniani, iliyoadhimishwa Septemba 16, huku kiwilaya zikifanyika katika ofisi za Mamlaka hiyo iliyoko jengo la ofisi ya Mkuu wa Wilaya
“Nimefurahi kupata elimu hii kwa sababu imetusaidia kuelewa umuhimu wa Kitambulisho cha Taifa. Ni muhimu kila mwananchi kuhakikisha anasajiliwa na kuwa na kitambulisho chake kwa sababu kinahitajika katika huduma mbalimbali, amesema Emily.
Ameongeza kuwa utoaji wa elimu kwa wananchi ni muhimu kwa kuwa unawasaidia kufahamu taratibu za usajili, utambuzi na namna ya kupata huduma mbalimbali zinazotolewa na NIDA.
Naye mwananchi mwingine aliyeshiriki katika maadhimisho hayo ameishukuru NIDA Kishapu kwa kuendelea kuwafikishia huduma wananchi, akisema hatua hiyo inarahisisha upatikanaji wa Vitambulisho vya Taifa bila wananchi kulazimika kufuata huduma hizo mbali na maeneo yao.

Katibu Tawala wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Fatma Mohamed
Kwa upande wake, wananchi wameendelea kuhamasishwa kutumia huduma zinazotolewa na NIDA na kuhakikisha taarifa zao za utambulisho zinakuwa sahihi na kusasishwa pale inapohitajika.
Siku ya Utambulisho Duniani huangazia umuhimu wa utambulisho wa kisheria katika kumtambua mtu na kuwezesha upatikanaji wa huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kauli mbiu “Utambulisho Wangu, Kivuli Changu. Havitengani!”, inayosisitiza umuhimu wa kila mwananchi kuwa na utambulisho rasmi.










Social Plugin