**
Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Mhe. Emmanuel Cherehani, ametoa wito mzito kwa viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS) kuhakikisha wanasimamia kwa uadilifu fedha za wakulima, kuwalipa kwa wakati na kuacha matumizi yoyote yasiyo sahihi ya fedha zinazotokana na jasho la wakulima.
Cherehani ametoa kauli hiyo Septemba 15, 2026, wakati wa kikao kilichowakutanisha viongozi wa vyama vya msingi vya tumbaku, vyama vya ushirika, taasisi za fedha pamoja na wadau mbalimbali wanaohusika na zao la tumbaku katika Halmashauri ya Ushetu, Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga.
Akizungumza katika kikao hicho, Cherehani amesema viongozi wa vyama vya ushirika wanapaswa kutambua kuwa nyuma ya kila fedha anayolipwa mkulima kuna jasho, muda, gharama na wakati mwingine mikopo ambayo mkulima ameitumia kuhakikisha anazalisha mazao yake.
“Natoa wito mzito kwa viongozi wote wa vyama vya ushirika: fedha ya mkulima si fedha ya chama, si fedha ya kiongozi, wala si fedha ya kutumia kwa matakwa binafsi. Ni jasho la mkulima na ni haki yake,” amesema Cherehani.
Amesema fedha ambayo mkulima anaisubiri baada ya kuuza mazao yake si fedha ya kawaida, bali ndiyo inayotegemewa kugharamia mahitaji muhimu ya familia, ikiwemo chakula, ada za watoto, matibabu, marejesho ya mikopo pamoja na kuandaa mtaji wa msimu unaofuata.
Kwa msingi huo, amesema kuchelewesha malipo ya mkulima bila sababu halali kunaweza kuathiri moja kwa moja maisha ya mkulima na familia yake, huku pia kukwamisha uwezo wake wa kuendelea na uzalishaji katika msimu unaofuata.
Mbunge huyo amesisitiza kuwa ucheleweshaji wa malipo, ukosefu wa uwazi kuhusu fedha za wakulima na matumizi yasiyo sahihi ya fedha za vyama vya ushirika ni masuala yanayopaswa kuchukuliwa kwa uzito na kushughulikiwa kwa mujibu wa taratibu na sheria.
“Kumcheleweshea mkulima malipo bila sababu halali, kutokuwa wazi kuhusu fedha zake au kutumia vibaya fedha za chama ni jambo linalopaswa kuchukuliwa kwa uzito mkubwa. Viongozi wa ushirika wamepewa dhamana na wanapaswa kuilinda dhamana hiyo,” amesema.
Amesema uongozi wa AMCOS haupaswi kutafsiriwa kama fursa ya kujinufaisha, bali ni dhamana ya kulinda maslahi ya wanachama na kuhakikisha mfumo wa ushirika unafanya kazi kwa manufaa ya mkulima.
Cherehani amewakumbusha viongozi hao kuzingatia Sheria ya Vyama vya Ushirika Na. 6 ya mwaka 2013, kanuni na masharti ya vyama vyao pamoja na maelekezo halali ya mamlaka husika, akisisitiza umuhimu wa uadilifu, uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa fedha na mali za wanachama.
Social Plugin