Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI ZA AFRIKA ZATAKIWA KUONGEZA BAJETI ZA AFYA KUELEKEA HUDUMA BORA KWA WOTE


Na Bora Mustafa,Arusha.

Serikali za Afrika na dunia zimetakiwa kuongeza bajeti kutoka kwenye mapato ya ndani kwa ajili ya sekta ya afya na kuhakikisha fedha zilizoidhinishwa zinatolewa kwa wakati, huku hatua zikichukuliwa kuelekea kufikia lengo la asilimia 15 ya matumizi ya serikali katika sekta ya afya.


Akifunga Mkutano wa Pili wa Kimataifa  Leo Ijumaa septemba 11,2026 wa Afya ya Msingi uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha, AICC, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange, kwa niaba ya Waziri wa TAMISEMI, Prof. Riziki Shemdoe, amesema uwekezaji katika afya msingi ni muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kwa usawa.

Dkt. Dugange amesema jitihada zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuimarisha huduma za afya ngazi ya msingi na rufaa zimeendelea kuifanya Tanzania kutambulika katika sekta ya afya barani Afrika, huku Rais Samia akitajwa kuwa kinara katika eneo la afya ya mama na mtoto.

Pia amesema nchi za Afrika zinapaswa kuunganisha nguvu na kufanya kazi kwa pamoja katika kutekeleza ajenda za afya zilizoridhiwa na viongozi wa Afrika na dunia, kwa kuhakikisha sera za afya msingi na afya kwa wote zinatekelezwa kwa vitendo.

Dkt. Dugange amesema hatua hiyo inapaswa kwenda sambamba na kuimarisha mnyororo wa ugavi wa dawa na bidhaa za afya, kuongeza upatikanaji wa rasilimali watu wenye ujuzi na mafunzo, pamoja na kuhakikisha ubora wa huduma katika vituo vya afya msingi.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo inayowasiliana na kuwezesha ubadilishanaji wa taarifa, hususan katika mifumo ya kliniki, bima, ufuatiliaji wa magonjwa, bidhaa za afya na programu maalumu.

Dkt. Dugange pia amesema ushiriki wa jamii katika kupanga, kutekeleza na kufuatilia huduma za afya ni muhimu ili kuhakikisha huduma hizo zinakidhi mahitaji halisi ya wananchi.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Afya TAMISEMI, Prof. Tumaini Nagu, amesema katika siku tatu za mkutano huo imebainika kuwa uwekezaji katika miundombinu na vifaa vya afya lazima uende sambamba na uwepo wa watumishi wenye ujuzi.

Pia Prof. Nagu amesema pamoja na miundombinu na vifaa, ni muhimu kuwepo kwa dawa, vifaa tiba, fedha za uendeshaji, matengenezo ya vifaa pamoja na matumizi sahihi ya mifumo ya kidijitali.

Amesema hatua hizo ni muhimu katika kuimarisha huduma za afya msingi na kufikia lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya kwa wote

Hata hivyo Wadau wa afya wameeleza kuwa huduma bora za afya zinapaswa kupatikana kwa usawa bila ubaguzi, bila kujali uwezo wa kifedha wa mwananchi au eneo analoishi.





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com