
Na Bora Mustafa, Arusha.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange kwaniaba ya Waziri wa TAMISEMI Prof. Riziki Shemdoe amesema jitihada zinazofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika sekta ya afya ngazi ya Msingi na Rufaa imesaidia kutambulika kwa Tanzania katika sekta ya afya Msingi barani Afrika na yeye Mwenyewe kuwa kinara katika afya ya mama na mtoto.
Dkt. Dugange amebainisha hayo leo Ijumaa Septemba 11, 2026 wakati akifunga Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Afya ya msingi kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha AICC, akihimiza kuendelea kuunganisha nguvu na kufanya kazi kwa pamoja ili kuendelea kuimarisha na kustawisha huduma ya afya msingi katika utekelezaji wa ajenda muhimu zilizoridhiwa na Viongozi wa Afrika na dunia kwa ujumla.
"Katika utekelezaji wake nisisitize kuwa ni muhimu Nchi za Afrika zielekeze nguvu katika kugharamia, kutekeleza na kusimamia sera za huduma za afya msingi na huduma kwa wote ili sera hizo zitafsiriwe kwa vitendo na kuleta huduma imara, mnyororo imara wa ugavi wa bidhaa za huduma za afya na kuimarisha upatikanaji na mafunzo ya rasilimali watu katika huduma za afya msingi na ubora wa bidhaa unaonekana katika vituo vya kutolea huduma ngazi ya afya ya msingi." Amesema Dkt. Dugange.
Aidha Dkt. Dugange amesisitiza umuhimu wa serikali za Afrika kuendelea kuongeza bajeti za mapato ya ndani ya sekta ya afya ili zilinde fedha hizo kwaajili ya huduma za afya ya msingi na kuhakikisha fedha zilizoizinishwa zinatolewa kwa wakati ili kuelekea kwenye lengo la Abuja la matumizi ya asilimia 15 ya matumizi ya serikali kwenye sekta ya afya.
Pia amesisitiza pia umuhimu wa kila mwananchi kupata huduma bora kwa usawa bila ubaguzi na kuathiriwa na mahali anapoishi au uwezo wake wa kifedha pamoja na Nchi za Afrika na dunia kuwa katika mfumo unaowasiliana na ubadilishanaji wa taarifa hususan uunganishaji wa mifumo ya kliniki, bima, ufuatiliaji wa magonjwa, bidhaa za afya na programu maalumu.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu (Afya)TAMISEMI Prof. Tumaini Nagu amesema katika siku tatu za mkutano huo wamebainisha kuwa uwekezaji katika miundombinu na vifaa lazima uende sambamba na watumishi wenye ujuzi, dawa, tiba, vifaatiba, fedha za uendeshaji, matengenezo pamoja na matumizi sahihi ya mifumo ya kidijitali katika kufikia huduma bora za afya kwa wote.




Social Plugin