Bodi ya Wakurugenzi ya Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) imekabidhi pikipiki kwa Kamati ya Watumia Maji Ngazi ya Jamii (CBWSO) ya MIMAKI, Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya, kwa lengo la kuongeza ufanisi katika utoaji na usimamizi wa huduma za maji kwa wananchi.
Pikipiki hiyo imekabidhiwa kwa niaba ya Bodi ya Wakurugenzi ya RUWASA na Mjumbe wa Bodi hiyo, Mhandisi Ngwisa Wilfred Mpembe, kwa chombo cha watoa huduma ya maji cha MIMAKI chenye makao makuu katika Kijiji cha Mpuguso, Kata ya Mpuguso.
MIMAKI inahudumia wananchi katika vijiji 14 vilivyopo katika kata za Mpuguso, Ilima, Malindo na Kisondela, eneo ambalo lina ukubwa wa kijiografia na hivyo kuhitaji usafiri wa uhakika kwa ajili ya ufuatiliaji na utatuzi wa changamoto za huduma ya maji.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mhandisi Mpembe aliwataka viongozi wa CBWSO kuhakikisha wanatumia chombo hicho kuongeza ufanisi wa huduma na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi kwa wakati.
Alisema pikipiki hiyo inapaswa kuwa chachu ya kuwafikia wananchi kwa urahisi, hususan katika kushughulikia changamoto ndogo ndogo zinazoweza kuathiri upatikanaji wa maji, ikiwemo upotevu wa maji katika maeneo mbalimbali.
“Hakikisha chombo hiki kinakuwa chachu ya kuwafikia wananchi na kupunguza changamoto ndogo ndogo kama za upotevu wa maji katika maeneo yenu,” alisema Mhandisi Mpembe.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa RUWASA Wilaya ya Rungwe, Wordson Pakyindi, alisema kupatikana kwa pikipiki hiyo kutarahisisha utoaji wa huduma katika eneo hilo kutokana na ukubwa wa kijiografia wa maeneo yanayohudumiwa na MIMAKI.
Alisema RUWASA itaendelea kuhakikisha huduma za maji zinaimarika kwa wananchi wa Wilaya ya Rungwe, huku ikisimamia vyombo tisa vinavyotoa huduma ya maji katika wilaya hiyo.
Hata hivyo, Pakyindi alieleza kuwa bado kuna uhitaji wa vyombo zaidi vya usafiri kutokana na ukubwa wa eneo la Rungwe na mahitaji ya ufuatiliaji wa miundombinu ya maji.
Makabidhiano hayo yalihudhuriwa na viongozi wa CBWSO, viongozi wa serikali za vijiji, wajumbe wa kamati za maji pamoja na wananchi ambao walipata fursa ya kutoa maoni kuhusu huduma za maji katika maeneo yao.
Wananchi waliishukuru RUWASA na Serikali kwa ujumla kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya maji na kutoa vifaa vya usafiri vinavyolenga kuimarisha usimamizi na utoaji wa huduma kwa jamii.
RUWASA imeendelea kusisitiza umuhimu wa kuimarisha uwezo wa vyombo vya huduma ya maji ngazi ya jamii ili kuhakikisha changamoto zinatatuliwa kwa wakati na wananchi wanapata huduma ya maji iliyo bora na endelevu.




Social Plugin