Mbunge wa Jimbo la Namtumbo na Waziri wa Katiba na Sheria Dkt.Juma Zuberi Homera akiwa anasikiliza na kuandika kero za wananchi wa jimbo lake katika vijiji vinne alivyovitembelea katika ziara yake ambapo atakua na siku nne ya ziara hiyo jimboni humo
Mwananchi wa kijiji cha Songambele Maimuna Adamu wa kata ya Mchomoro akitoa kero yake kwa Mbunge wa Jimbo la Namtumbo na Waziri wa Katiba na Sheria Dkt.Juma Zuberi Homera 
Mbunge wa Jimbo la Namtumbo na Waziri wa Katiba na Sheria Dkt.Juma Zuberi Homera akimkabidhi diwani wa kata ya Mchomoro bi Rehema Chiku Katikula fedha taslimu kiasi cha shilingi milioni tano kwa wanawake wajasiriamali wadogo katika kijiji cha Mingweha kilichopo Kata ya Mchomoro Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo
Na Regina Ndumbaro
Namanima-Namtumbo
Wananchi wa Kijiji cha Namanima, Jimbo la Namtumbo mkoani Ruvuma, wamemweleza Waziri wa Katiba na Sheria na Mbunge wa Jimbo la Namtumbo, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, changamoto ya ukosefu wa maji ambayo wamesema imekuwa ikiwasumbua kwa miaka mingi.
Wakizungumza katika ziara yake ya kusikiliza kero za wananchi, Mariamu Mbaraka na Imani Shaibu Matumbi kwa niaba ya wananchi, wamesema hali hiyo inawalazimu wanawake kuamka alfajiri na kutembea umbali mrefu kutafuta maji, huku dumu moja likigharimu Sh800.
Wananchi hao pia wameomba hatua zichukuliwe kuboresha huduma za afya na miundombinu ya barabara, wakieleza kuwa baadhi ya wanawake wajawazito hulazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya na wakati mwingine kujifungulia njiani.
Wamesema changamoto hiyo inaweza kuhatarisha maisha ya mama na mtoto, hivyo wameomba kujengewa zahanati pamoja na kurekebishiwa barabara.
Aidha, wamewasilisha changamoto za umeme na eneo la hifadhi, wakieleza matumaini yao kuwa ziara ya Dkt. Homera itasaidia kupata ufumbuzi wa kero hizo.
Akijibu kero hizo, Dkt. Homera amesema anafahamu kuwa maji ni changamoto kubwa Namanima na kwamba suala hilo lilishawasilishwa kwake na Diwani.
Amesema ametenga Sh milioni 1.6 kwa ajili ya kununua pampu na tenki ili kuwawezesha wananchi kupata huduma hiyo, huku akiwataka wananchi kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwa hatua zinazochukuliwa katika kuwaletea maendeleo.
Pia amesema amebaini umuhimu wa zahanati katika eneo hilo kutokana na umbali uliopo na ameahidi kulifanyia kazi pamoja na changamoto ya shule iliyochakaa.
Kwa upande wa barabara, Dkt. Homera alimpa nafasi Meneja wa TARURA Wilaya ya Namtumbo, Mhandisi Fabian Lugaraba, kueleza hatua zinazochukuliwa.
Mhandisi Lugaraba amesema kwa mujibu wa utaratibu, barabara inapofanyiwa ukarabati mkubwa hudumu takribani miaka mitatu kabla ya kurejea kufanyiwa matengenezo, hivyo barabara ya Namanima–Masuguru imepangwa kufanyiwa ukarabati mwakani.
Amesema uchunguzi umebaini kuwa barabara hiyo ina kifusi kisichokuwa na ubora unaohitajika, hivyo TARURA imeandaa kifusi kingine kitakachochukuliwa Migeregere na kuwekwa katika barabara hiyo, hatua inayotarajiwa kuondoa changamoto zilizojitokeza.






Social Plugin