Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MUSA RYOBA ATWAA TUZO MBILI KUTAMBUA MCHANGO WAKE KATIKA MAENDELEO YA JAMII


Mkurugenzi na Mwanzilishi wa Mwanzo Mpya Foundation,Musa Ryoba ametwaa tuzo mbili tofauti zinazotambua mchango wake binafsi pamoja na kazi zinazofanywa na taasisi hiyo katika maendeleo ya jamii.

Tuzo hizo zimetolewa na taasisi ya HolySmile, ambapo Ryoba ametunukiwa Tuzo ya Mwanasiasa Bora Kijana na Mchango katika Maendeleo ya Jamii – 2026, huku Mwanzo Mpya Foundation ikitunukiwa Tuzo ya Taasisi Bora Chipukizi yenye Mchango Chanya katika Jamii – 2026.

Kwa Ryoba, tuzo hizo mbili zimekuja katika nafasi mbili tofauti, ambapo moja imetolewa kwa kutambua mchango wake kama mwanasiasa kijana, huku nyingine ikiwa ni utambuzi wa kazi anazofanya kupitia nafasi yake kama Mkurugenzi na Mwanzilishi wa Mwanzo Mpya Foundation.

Akielezea ushindi huo, Ryoba amesema tuzo hizo ni sehemu ya utambuzi wa safari yake katika kushiriki shughuli zinazolenga kuleta mabadiliko katika jamii.

Mwanzo Mpya Foundation ni taasisi inayojihusisha na shughuli za kijamii, ikilenga kuchangia katika kuboresha maisha ya wananchi kupitia programu mbalimbali zinazogusa mahitaji muhimu ya jamii.

Miongoni mwa maeneo ambayo taasisi hiyo imekuwa ikiyapa kipaumbele ni uwezeshaji wa vijana na wanawake, afya, upatikanaji wa maji safi na salama, elimu, ujuzi pamoja na masuala mengine yanayohusu maendeleo ya jamii.

Kupitia programu zake, taasisi hiyo imekuwa ikishirikiana na jamii katika kutambua changamoto zinazowakabili wananchi na kutafuta namna ya kuzitatua kwa kutumia rasilimali na fursa zilizopo.

Taasisi hiyo inalenga zaidi jamii zilizo katika mazingira yenye changamoto, huku vijana na wanawake wakiwa miongoni mwa makundi yanayolengwa kupitia shughuli zake.

Tuzo hizo zimetolewa na HolySmile, taasisi inayohusika na shughuli mbalimbali ikiwemo programu za tuzo zinazolenga kutambua na kuthamini mchango wa watu binafsi, taasisi na wadau mbalimbali katika jamii.

Kupitia Mdau Shupavu Awards, HolySmile imekuwa ikitambua mchango wa wadau katika maeneo mbalimbali ya kijamii, kiuchumi, kielimu, kiafya, kiutamaduni na mengine yenye umuhimu kwa jamii.

Tuzo hizo zinalenga pia kuhamasisha watu na taasisi kuendelea kutumia vipaji, uwezo na nafasi zao kuleta matokeo chanya katika jamii.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com