Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DKT. NGUVILA : ARUSHA IMEJIPANGA KUKABILIANA NA MADHARA YA EL NINO


Na Mwandishi Wetu- Arusha
 
Katibu Tawala Mkoa wa Arusha Dkt. Toba Nguvila amesema, Mkoa wa Arusha umejipanga vyema katika kuchukua hatua za kukabiliana na madhara ya El nino zinazotarajiwa kuanza mwezi Oktoba 2026.
 
Dkt. Nguvila ameyasema hayo leo Septemba 30, 2026 wakati wa Kikao Kazi cha Kujadili Utekelezaji wa Maelekezo yaliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na wenye Ulemavu) kwa Mikoa kuhusu Kujiandaa na Kukabiliana na Madhara ya El Niño kilichofanyika katika Ofisi za Mkuu wa Mkoa Arusha.
 
“Mkoa wa Arusha umekaa na kujipanga kikamilifu dhidi ya majanga yanayoweza kusababishwa na madhara ya mvua za El nino, aidha, mkoa umeanza kufanya tathmini katika maeneo hatarishi, kufanya usafi kuzibua mitaro, kulinda miundombinu ya utalii ambapo Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro na Mamlaka za barabara zimeagizwa kukagua na kukarabati mifumo ya mifereji, barabara na madaraja” ,amefafanua Dkt. Nguvila.
 
Akieleza taarifa ya jumla ya Mkoa, Mratibu wa Maafa Mkoa wa Arusha Bi. Asha Kipingu amebainisha kuwa kufuatia taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini (TMA) za kuwepo kwa mvua za Eli nino, Mkoa wa Arusha umefanya jitihada na hatua mbalimbali ili kupunguza/kuzuia athari ikiwa na pamojja na kufanyia kazi maelekezo ya Ofisi ya Waziri Mkuu-SBUU
 
“Katika kuandaa rasilimali kwa ajili ya kuzuia au kupunguza madhara, kujiandaa na kukabiliana na maafa yanayoweza kutokea tayari TANROADS imepokea vifaa vya dharura makalvati ya chuma 300, gabions 100 na Reno Mattresses 40, aidha,TARURA imetengewa fedha kwa ajili ya kununua na kuweka makalvati ya plastic lakini pia Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro imeunda kamati ya wataalamu kutoka sehemu za huduma ya ulinzi, uhandisi, nyanda za malisho na utafiti, maendeleo ya jamii na utalii kwa ajili ya kuratibu maandalizi kabla, wakati na baada ya mvua za El nino zinazotarajiwa”, amefafanua Bi. Kipingu.
 
Aidha, amebainisha kuwa, elimu juu ya wananchi kuchukua tahadhari ya mvua za El nino, kutunza chakula na kufanya shughuli za kiuchumi maeneo salama kuepuka madhara ya athari ya mvua hiyo  imetolewa  kupitia mikutano ya vijiji, vikao mbalimbali vvilifanywa na Mkuu wa Mkoa, na Kamati ya Ulinzi na usalama ya Mkoa, wakuu wa Wilaya, wakurugenzi, wabunge wa viti maalum na Taasisi za Serikali zikiwemo TARURA,TANROAD,RUWASA ,AUWSA, TANESCO, TMA, REDCROSS, na kutoa maelekezo ya kukabiliana na athari za mvua hizo.
 
Vilevile, ameongeza kuwa, Halmashauri za mkoa wa Arusha zimetenga maeneo maalum kwa ajili ya makazi ya muda pindi maafa yatakapotokea lakini pia amesema agenda ya El nino imekuwa ikiongelewa kwenye kila vikao vinavyofanyika katika Mkoa wa Arusha ili kuwakumbusha wananchi kuwa tayari muda wote na Mvua hizi lakini pia kuchukua tahadhari.
 
Awali, akiwasilisha mada kuhusu hatua za zuchukua katika Kujiandaa na Kukabiliana na Madhara ya El Niño, Mratibu wa Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Bw. Fadhili Bagilo amebainisha kuwa, Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikisha wizara, taasisi, Mamlaka za Mikoa, Mashirika ya Kiserikali na yasiyo ya Serikali iliratibu maandalizi ya Mpango wa Dharura wa Taifa wa Kukabiliana na Madhara ya El Nino kwa kipindi cha Julai, 2026 hadi Juni, 2027.
 
“Mipango iliyoandaliwa katika ngazi za mikoa, wizara na taasisi ilijumishwa katika maadalizi ya mpango wa taifa, pia rasilimali za utekezaji wa mpango huu zitatoka katika bajeti za sekta husika” ameongeza Bw. Bagilo.
 
Aidha, ameeleza kuwa, majukumu katika usimamizi wa maafa  yamegawanywa katika kongani 15 ambapo kila kongani ina jukumu mahsusi linalopaswa kuratibiwa na kutekelezwa na idara au taasisi yenye jukumu hilo kwa mujibu wa katiba, sheria, miongozo au miundo ya serikali iliyopo.
 
Usimamizi wa maafa ni jukumu letu sote, kila mmoja ashiriki sasa na kuchukua hatua katika eneo lake ili kuokoa na kulinda maisha, mali, miundombinu na mazingira










Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com