Waziri wa Katiba na Sheria Dkt.Juma Zuberi Homera (Mb)akiwa anazungumza na wananchi wa Namtumbo wakati wa ufunguzi wa kampeni hiyo inayotekelezwa kwa siku tatu Na Regina Ndumbaro, Namtumbo-Ruvuma
Wananchi wa Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, hususani wanaokabiliwa na changamoto za migogoro kati ya wakulima na wafugaji, wameanza kupata fursa ya huduma za msaada na elimu ya kisheria kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia Awamu ya Pili, iliyofunguliwa rasmi leo Septemba 17, 2026, na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera (Mb), katika viwanja vya ushirika, wilaya ya Namtumbo.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kampeni hiyo inayotekelezwa kwa siku tatu, Mhe. Dkt. Homera amesema uwepo wa kampeni hiyo Namtumbo umetokana na ombi maalum la wananchi waliotaka huduma za msaada na elimu ya kisheria, kutokana na changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo, ikiwemo migogoro ya mara kwa mara kati ya wakulima na wafugaji.
Amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi na kutumia fursa hiyo kupata ushauri na msaada wa kisheria kutoka kwa wataalamu waliopo.
Amesema wananchi watapata huduma mbalimbali ikiwemo ushauri na usuluhishi wa masuala ya ardhi na mirathi, ndoa na madai, matunzo ya watoto, ukatili wa kijinsia, elimu ya kisheria na uwakilishi mahakamani, pamoja na utoaji wa vyeti vya kuzaliwa na uandaaji wa nyaraka mbalimbali za kisheria.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Wilaya ya Namtumbo, Ndg. Francis George Mgoloka, amewahimiza wananchi kutumia kikamilifu kampeni hiyo kwa kuwasilisha changamoto zao na kupata elimu ya kisheria.
Kampeni hiyo yenye ujumbe “Msaada wa Kisheria kwa Haki, Usawa, Amani na Maendeleo,” inalenga kusogeza huduma za msaada wa kisheria karibu na wananchi wa Namtumbo, wakiwemo wakulima na wafugaji wanaokumbwa na migogoro ya matumizi ya ardhi, ili kupata elimu, ushauri na huduma za kisheria zinazoweza kusaidia katika kushughulikia changamoto zao kwa njia zinazotambua haki na taratibu za kisheria.





Social Plugin