Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MADINI YAIBUA FURSA ZA KIUCHUMI LINDI PROFESA SHEMDOE



Na Sheila Ahmadi, Ruangwa

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Profesa Riziki Shemdoe amesema fursa zinazotokana na sekta ya madini nchini zina mchango mkubwa katika kuchochea ukuaji wa uchumi na maendeleo.

Profesa Shemdoe ameyasema hayo baada ya kufungua Maonyesho ya Madini yanayofanyika mkoani Lindi, maarufu kama Mining Expo 2026 ambapo amesema mkoa huo una fursa mbalimbali za madini zinazoweza kuongeza shughuli za kiuchumi na kuwanufaisha wananchi Mkoani humo.

Aidha Mkoa wa Lindi ina utajiri wa madini mbalimbali, ikiwemo dhahabu, nikeli na madini mengine, hivyo ni muhimu kuendelea kuweka mazingira yanayowawezesha wadau kushiriki katika sekta hiyo.

“Serikali inatambua mchango mkubwa wa sekta ya madini katika kuchochea uongezaji wa thamani wa madini yanayopatikana nchini. Hivyo, tutaendelea kushirikiana na taasisi zinazohusika na sekta ya madini, sekta binafsi pamoja na wachimbaji wa madini,” amesema Profesa Shemdoe.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Adam Malima, amesema Mkoa wa Lindi ni miongoni mwa maeneo yenye uzalishaji wa madini hali inayochangia kuongeza shughuli za kiuchumi na upatikanaji wa malighafi zinazotokana na rasilimali hizo.

Malima amesema uwepo wa shughuli za uchimbaji wa madini mkoani humo unaendelea kutoa fursa za kiuchumi kwa wananchi na kuchangia katika kuongeza uzalishaji na mapato ya nchi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com