Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

LINDI JUMBO YAFUNGUA FURSA ZA AJIRA KWA WAZAWA




Na Sheila Ahmadi, Ruangwa


Kampuni ya Lindi Jumbo inayojihusisha na uchimbaji wa madini mkoani Lindi imesema asilimia 93 ya wafanyakazi wake ni Watanzania wazawa, hatua inayowezesha wananchi wa maeneo yanayozunguka mgodi kunufaika na fursa za ajira zinazotokana na shughuli za uchimbaji madini.

Meneja wa Mgodi wa Lindi Jumbo, Frank Isenge, amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Maonyesho ya Madini yanayofanyika wilayani Ruangwa, mkoani Lindi, ambapo amesema kampuni hiyo inaendelea kutoa fursa za ajira kwa wananchi, hususan wanaoishi katika maeneo ya jirani na mgodi.

Amesema ajira hizo ni sehemu ya mchango wa kampuni katika kukuza uchumi wa jamii inayozunguka mgodi, huku akisisitiza kuwa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi ni muhimu katika kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi.

“Tunashirikiana na Serikali kupitia sekta ya madini katika kuhakikisha shughuli zetu zinakuwa na manufaa kwa jamii. Maonyesho haya pia ni fursa muhimu ya kuitangaza kampuni na shughuli tunazofanya,” amesema Isenge.

Aidha, Isenge amesema kampuni hiyo imeshiriki katika Maonyesho ya Madini kwa zaidi ya mara tatu, ikiwa pia imekuwa miongoni mwa wadhamini wa maonyesho hayo.

Kwa upande wake, Afisa Rasilimali Watu wa kampuni hiyo, Adam Komba, amesema kati ya wafanyakazi wazawa wanaofikia asilimia 93, sehemu kubwa wanatoka katika maeneo mbalimbali ya mkoani Lindi, ikiwemo Ruangwa, Liwale na Nachingwea.

Amesema hali hiyo imeendelea kuwawezesha wananchi wa maeneo hayo kupata ajira na kunufaika moja kwa moja na shughuli za kampuni hiyo.

“Wafanyakazi wengi wazawa wanatoka katika maeneo jirani na mgodi, ikiwemo Ruangwa, Liwale na Nachingwea. Hivyo, kupitia shughuli za mgodi, wananchi wameendelea kupata fursa za ajira na kunufaika kiuchumi,” amesema Komba.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com