Na Sheila Ahmadi, Geita
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imewahamasisha wawekezaji kutumia fursa ya ujenzi wa vituo vya mafuta vya gharama nafuu katika maeneo ya vijijini, ikiwa ni hatua ya kuongeza upatikanaji wa huduma za nishati na kupunguza uuzaji holela wa bidhaa za mafuta.
Akizungumza katika Maonesho ya Tisa ya Madini yanayofanyika katika Viwanja vya Samia Suluhu Hassan, mkoani Geita, Meneja wa EWURA Kanda ya Ziwa Mhandisi Nyirabu Musira amesema mamlaka hiyo imekuja kwenye maonesho hayo kutoa elimu kwa wananchi, wawekezaji na wadau kuhusu huduma inazozidhibiti pamoja na fursa zilizopo katika sekta ya nishati.
Aidha moja ya maeneo ambayo EWURA imeweka mkazo ni kuhamasisha uwekezaji katika vituo vya mafuta vijijini, ambapo masharti na gharama za leseni zimepunguzwa ili kurahisisha wananchi na wawekezaji kuingia katika biashara hiyo.
gharama ya kuomba leseni ya kituo cha mafuta mjini ni Sh50,000, na kwa maeneo ya vijijini pia ni Sh50,000. Hata hivyo, gharama ya leseni ya miaka mitano kwa kituo cha mjini ni Sh1 milioni, wakati kwa kituo cha vijijini ni Sh100,000,” amesema.
Amesema hatua hiyo imepunguza kwa kiasi kikubwa gharama za uwekezaji, huku EWURA ikiwa imerahisisha pia masharti ya ujenzi wa vituo hivyo ili visilazimike kuwa na muonekano na miundombinu inayofanana na vituo vikubwa vilivyopo mijini.
“Kwa maeneo ya vijijini hatulazimishi sana kituo kiwe na muonekano na mfanano wa vituo vya mjini ili gharama za uwekezaji ziwe chini,” amesema.
Musira ameongeza kuwa lengo la hatua hiyo ni kuongeza upatikanaji wa huduma za mafuta vijijini na kupunguza au kuondoa kabisa uuzaji holela wa bidhaa za petroli ambao unaweza kuhatarisha usalama wa wananchi.
Aidha, amesema EWURA imetumia maonesho hayo kutoa elimu kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa kuhamasisha matumizi ya nishati hiyo.
Kupitia mamlaka hiyo inaendelea kutoa elimu kuhusu uvunaji wa maji ya mvua, hususan kutokana na matarajio ya kuanza kwa msimu wa mvua, ambapo wananchi wanahimizwa kutumia maji hayo kama njia mbadala kwa matumizi mbalimbali.
Kwa upande wake Ofisa Uhusiano kutoka Mamlaka ya udhibiti wa huduma za nishati na maji(EWURA) Tobietha Makafu amewataka mafundi umeme ambao bado hawana leseni kufika katika banda la mamlaka hiyo ili kupata elimu kuhusu taratibu za kupata leseni na kufanya kazi kwa mujibu wa sheria.
Vilevile EWURA inapokea na kushughulikia malalamiko ya wananchi kuhusu huduma za nishati na maji zinazodhibitiwa na mamlaka hiyo.
kuhusu huduma ya maji na umelalamika kwenye mamlaka husika lakini hujasikilizwa, au una malalamiko kuhusu TANESCO na hujapata ufumbuzi, tuko hapa katika maonesho haya kupokea malalamiko yako na kuyafanyia kazi,” amesema.
EWURA imewahimiza wananchi wa Geita na mikoa mingine ya Kanda ya Ziwa kutembelea banda lake katika maonesho hayo ili kupata elimu kuhusu huduma za nishati na maji, taratibu za kupata leseni, fursa za uwekezaji pamoja na namna ya kuwasilisha malalamiko na kupata ufumbuzi.

Social Plugin