Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

B.O.T YAWAASA WANANCHI KUJIHADHARI NA NOTI BANDIA



Na Sheila Ahmadi, Ruangwa

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Tawi la Mtwara imewataka wananchi kujifunza alama za usalama zilizowekwa kwenye noti za Tanzania ili waweze kutambua fedha halali na kujikinga na hasara inayoweza kusababishwa na noti bandia.

Wito huo umetolewa na Meneja Msaidizi wa Huduma za Kibenki wa BoT, Tawi la Mtwara, Emmanuel Alfred Kasupa, wakati akizungumza na Wanahabari kwenye banda la benki hiyo katika Maonyesho ya Madini na Fursa za Uwekezaji yanayofanyika Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, mkoani Lindi.

Kasupa amesema wananchi wanapaswa kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu alama za usalama zilizopo kwenye noti, kwa kuwa hatua hiyo inaweza kuwasaidia kugundua fedha bandia kabla ya kuzitumia katika shughuli zao za kila siku.

Noti halali zina alama mbalimbali za usalama ambazo zinaweza kuchunguzwa kwa kutumia macho, kwa kugusa baadhi ya sehemu za noti na kwa kutumia vifaa maalumu vya mwanga wa ultraviolet (UV).

“Tunatoa elimu kuhusu namna ya kutambua alama zilizopo katika noti halali za Tanzania, utunzaji mzuri wa noti na sarafu pamoja na usimamizi wa fedha binafsi,” amesema Kasupa.

elimu hiyo ni muhimu hasa katika kipindi ambacho wananchi wanashiriki katika shughuli mbalimbali za biashara, ambapo fedha hubadilishana mikono mara kwa mara.

“Tunasisitiza wananchi kujifunza alama za usalama zilizowekwa kwenye noti, kwa sababu wanapokuwa na uelewa huo ni rahisi kutambua noti halali na kuepuka hasara inayoweza kusababishwa na noti bandia,” amesema.

Mbali na elimu ya utambuzi wa noti, Kasupa amesema BoT inawahimiza wananchi kuwa na nidhamu katika matumizi ya fedha kwa kupanga matumizi kulingana na kipato wanachopata.

Kwa Upande Wake Afisa wa B.O.T tawi la Mtwara Beni Mgole Ameongeza kuwa baadhi ya watu hupokea kipato, ikiwemo mishahara, lakini hukitumia bila mpango na hivyo kukikosa kabla ya kufikia mwisho wa mwezi.

Aidha wananchi wanapaswa kutenga fedha kwa ajili ya mahitaji muhimu na kuweka sehemu ya kipato kwa matumizi ya baadaye ili kuongeza uwezo wa kukabiliana na mahitaji mbalimbali.

Vilevile amesema BoT inatoa elimu kuhusu matumizi ya mifumo ya malipo ya kidijitali, ambayo inaweza kurahisisha miamala na kupunguza utegemezi wa fedha taslimu katika shughuli mbalimbali.

Katika Hatua nyingine Ameongeza wananchi wanaweza kutumia mifumo hiyo katika kufanya malipo yanayohusiana na biashara na huduma mbalimbali, ikiwemo shughuli za ardhi mazao korosho na samaki.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com