Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WIZARA YA KATIBA NA SHERIA YATOA TAHADHARI DHIDI YA MATAPELI WANAOJITAMBULISHA KWA JINA LA WAZIRI



Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Wizara ya Katiba na Sheria imetoa tahadhari kwa wananchi kuhusu uwepo wa matapeli wanaotumia jina la Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Zuberi Homera, kuwaomba fedha kwa njia ya simu, huku ikisisitiza kuwa Waziri huyo hajawahi kuwasiliana na mtu yeyote kwa lengo la kuomba fedha.

Katika taarifa kwa umma iliyotolewa Agosti 5, 2026, Wizara imesema imepokea taarifa za mtu anayepiga simu kupitia namba 0623 728 828 na kujitambulisha kuwa ni Dkt. Homera, akiwataka wananchi watume fedha kwake au kwa ndugu zake kwa madai ya kugharamia msiba.

Wizara imefafanua kuwa namba hiyo si ya Waziri wa Katiba na Sheria na kwamba anayeitumia ni tapeli anayelenga kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Kutokana na hali hiyo, wananchi wametakiwa kuwa makini na kutuma taarifa za matukio kama hayo kwa kupiga namba ya huduma kwa umma 15040 mara wanapopigiwa simu za aina hiyo. Wizara imeeleza kuwa taarifa hizo zitafanyiwa kazi kwa ushirikiano na Jeshi la Polisi, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) pamoja na watoa huduma za mawasiliano.

Aidha, wananchi wanaohitaji kutoa taarifa kuhusu matukio hayo wanaweza kuwasiliana na Wizara ya Katiba na Sheria kupitia namba 0800-004-004, 0262-160-360 au WhatsApp 0739 101 910.

Wizara imewahimiza wananchi kuwa waangalifu dhidi ya matapeli wanaotumia majina ya viongozi wa Serikali kwa lengo la kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com