Na Dotto Kwilasa,Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI),Prof. Riziki Shemdoe amewataka viongozi na watendaji wa Serikali za Mitaa kuacha migogoro ya kiutendaji na badala yake kushirikiana katika kutekeleza majukumu yao, akisema hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana katika mazingira yenye migogoro.
Waziri huyo ametoa kauli hiyo leo Agosti 21,2026 wakati akifunga Mkutano Mkuu wa 16 wa Taasisi ya Maboresho katika Mamlaka za Serikali za Mitaa (TOA), ambapo amesisitiza kuwa mshikamano, kuheshimiana na kutambua mipaka ya mamlaka ni muhimu katika kuhakikisha Serikali za Mitaa zinatoa huduma bora kwa wananchi.
“Mahali ambapo kuna migogoro hakuna maendeleo, wala hapawi mahali pazuri pa kufanyia kazi,” amesema.
Kutokana na hayo amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri, Makatibu Tawala wa Wilaya, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakuu wa Mikoa kuheshimu mamlaka na mipaka ya majukumu ya kila mmoja ili kuondoa migongano inayoweza kuchelewesha utekelezaji wa mipango ya maendeleo.
Waziri Shemdoe amesema viongozi wanapaswa kuelekeza nguvu zao katika kutekeleza majukumu waliyopewa badala ya kutumia muda mwingi katika migogoro .
Akizungumzia suala hilo kwa kutumia uzoefu wake wa uongozi, amesema amewahi kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri na Katibu Tawala wa Mkoa, lakini katika nyadhifa hizo alijitahidi kuepuka migogoro na viongozi aliokuwa akifanya nao kazi.
Amesema viongozi wanapaswa kutambua kuwa nafasi za uongozi hubadilika na kwamba watu wanaofanya kazi pamoja leo wanaweza kukutana tena katika mazingira mengine ya kijamii au kiutumishi.
Katika hatua nyingine, Waziri Shemdoe amesema utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 hauwezi kuwa jukumu la Serikali Kuu pekee, akisisitiza kuwa Serikali za Mitaa zina nafasi kubwa katika kufanikisha malengo hayo.
Amesema utekelezaji wa Dira hiyo unapaswa kushuka hadi ngazi ya kata na vijiji ambako wananchi wanaguswa moja kwa moja na huduma na miradi ya maendeleo na hivyo kuzielekeza mamlaka husika kuangalia namna ya kuimarisha ujenzi wa uwezo kuanzia ngazi ya kata hadi vijiji, ili viongozi na watendaji wawe na uelewa na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa Dira 2050.
Aidha, ameziagiza mamlaka za Serikali za Mitaa kuandaa mikutano ya uelimishaji kuhusu Dira 2050 katika ngazi za mkoa, wilaya, halmashauri, kata na vijiji ili wananchi na wadau wa maendeleo waelewe nafasi yao katika utekelezaji wa Dira hiyo.
Waziri Shemdoe pia amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Serikali za Mitaa, akisema mamlaka hizo zina uwezo wa kuongeza mapato na kuyatumia katika miradi yenye manufaa kwa wananchi.
Amesema Serikali imeweka lengo la kukusanya Sh1.9 trilioni katika mapato ya ndani, huku akizitaka mamlaka za Serikali za Mitaa kuongeza juhudi ili kufikia na kuvuka lengo hilo.
“Tuendelee kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani, lakini vilevile kufanya miradi ambayo inaonekana kutokana na mapato tunayoyakusanya,” amesema.
Waziri Shemdoe pia ameelekeza Serikali za Mitaa kuendelea kuimarisha maeneo saba muhimu, ikiwemo utoaji wa huduma bora unaozingatia mahitaji halisi ya wananchi, ukusanyaji na usimamizi wa mapato ya ndani, pamoja na uwajibikaji na uadilifu katika matumizi ya rasilimali za umma.
Maeneo mengine ni matumizi ya TEHAMA na ubunifu katika kuboresha utendaji, ushirikishwaji wa wananchi katika kupanga na kusimamia shughuli za maendeleo, pamoja na kujenga uwezo wa viongozi na watendaji wa Serikali za Mitaa.
Amesema Serikali iko tayari kuendelea kushirikiana na TOA katika maeneo yenye maslahi mapana kwa taifa, ikiwemo kubadilishana uzoefu na mbinu bora za uongozi, kujenga uwezo wa viongozi na watendaji, kufanya tafiti na kutoa ushauri wa kitaalamu kuhusu Serikali za Mitaa.
Aidha Waziri Shemdoe amewataka washiriki wasirejee katika maeneo yao wakiwa na kumbukumbu za mkutano pekee, bali warejee na hatua za utekelezaji.
Amesema tija ya mkutano hupimwa kwa utekelezaji wa maazimio, mapendekezo na maarifa yanayopatikana, hivyo viongozi na watendaji wanapaswa kuhakikisha yaliyokubaliwa yanafanyiwa kazi kwa kuzingatia mamlaka na majukumu ya kila mmoja.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TOA Albert Msovela amesema mkutano huo umefanyika baada ya maboresho ya Katiba ya TOA yaliyowezesha Makatibu Tawala wa Wilaya (DAS) kuwa sehemu ya wajumbe wa chama hicho.
Amesema marekebisho hayo yalitokana na azimio la Mkutano Mkuu wa 14 uliofanyika Arusha, huku Mkutano Mkuu wa 16 ukiwa wa kwanza kushirikisha rasmi kundi hilo.
Mwenyekiti huyo amesema kaulimbiu ya mkutano huo imejikita katika “Ugatuzi wa madaraka katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ni nguzo madhubuti ya kufikia Dira ya Taifa ya 2050.”
Aidha, ameiomba Serikali kuendelea kutoa msukumo katika utekelezaji wa sera ya Ugatuzi wa Madaraka, maarufu D by D, akisema utekelezaji wake ni muhimu katika kufanikisha malengo yaliyowekwa kwenye Dira 2050.
Amesema TOA itaendelea kushirikiana na Serikali katika kusimamia rasilimali za umma, watumishi, sheria, kanuni na miongozo, ukusanyaji wa mapato, utoaji wa huduma, uwekezaji na miradi ya maendeleo.
Pamoja na mambo mengine ,Mkutano huo ulihusisha pia wadau mbalimbali wa maendeleo, wakiwemo JICA, NMB, CRDB na taasisi nyingine zilizotajwa kuwa sehemu ya ushirikiano katika kuimarisha shughuli za TOA.








Social Plugin