Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeiomba Serikali kuongeza ruzuku kwa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), ili kuwezesha kuongeza kasi ya ujenzi wa nyumba za makazi ya watumishi wa umma nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Selemani Kakoso, wakati wa ziara ya kukagua miradi ya nyumba za watumishi inayotekelezwa na TBA katika maeneo ya Kisasa na Nzuguni jijini Dodoma, ikiwa ni sehemu ya ziara ya kutathmini utekelezaji wa miradi ya miundombinu nchini.
Kakoso amesema Kamati imejiridhisha na juhudi zinazofanywa na Serikali pamoja na TBA katika kukabiliana na changamoto ya makazi kwa watumishi wa umma, huku akisisitiza umuhimu wa kuongeza kasi ya ujenzi kutokana na mahitaji makubwa ya nyumba nchini.
Amesema eneo la Nzuguni lenye takribani ekari 630 lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa makazi ni hatua muhimu katika kuendeleza mji mpya wa Serikali, kwa kuwa uwepo wa nyumba hizo utawasaidia watumishi, wakiwemo walio katika ngazi za chini, kupata makazi yaliyo karibu na maeneo yao ya kazi.
“Tunawapongeza Serikali kwa juhudi kubwa zilizofanyika na pia TBA kwa mipango mizuri ya kuandaa nyumba za makazi ya watumishi. Tumekagua eneo la Kisasa na tumeona maboresho makubwa katika nyumba zilizojengwa,” amesema Kakoso.
Hata hivyo, Kamati imeishauri Serikali kuharakisha upatikanaji wa wabia kupitia utaratibu wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), ili kuongeza uwezo wa TBA kutekeleza miradi mikubwa ya nyumba kwa wakati na kukidhi mahitaji ya watumishi.
Kwa mujibu wa Kamati hiyo, ushirikishwaji wa sekta binafsi utawezesha kupatikana kwa mitaji na utaalamu zaidi, huku Serikali ikiendelea kusimamia miradi hiyo kuhakikisha inatoa huduma bora na nyumba zenye viwango vinavyokidhi mahitaji ya watumishi.
Kuhusu huduma ya maji, Kamati imepongeza TBA kwa kuanzisha mfumo wake wa maji bila kutegemea kikamilifu huduma kutoka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA).
Hata hivyo, imeitaka TBA kuongeza juhudi za kuchimba visima na kuimarisha mifumo ya majitaka ili kukidhi mahitaji ya eneo hilo kwa muda mrefu.
Aidha, Kamati imeishauri TBA kuangalia uwezekano wa kutumia nishati ya jua kama chanzo mbadala cha umeme, hatua ambayo itasaidia kupunguza utegemezi wa mfumo wa kawaida wa umeme na kuhakikisha huduma zinaendelea kupatikana wakati changamoto za umeme zinapotokea.
Vilevile, Kamati imeitaka Wizara ya Ujenzi kushirikiana na Ofisi ya Rais-TAMISEMI, TANROADS, TARURA pamoja na TBA katika ujenzi wa miundombinu bora ya barabara katika maeneo hayo, hususan barabara za lami, ili kuongeza mvuto wa makazi hayo na kurahisisha usafiri.
Kamati imesisitiza kuwa ujenzi wa nyumba za watumishi ni uwekezaji wa muda mrefu unaopaswa kuzingatia thamani ya fedha, ubora wa majengo na mahitaji ya wananchi, ili miundombinu hiyo iwe na tija kwa Serikali na kizazi cha sasa na kijacho.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Miliki wa TBA, Said Rajabu Mndeme, aliyemwakilisha Mtendaji Mkuu wa TBA, amesema mradi huo unatekelezwa katika eneo lenye takribani ekari 640, ambapo ujenzi wa nyumba 150 tayari umekamilika.
Amesema nyumba nyingine 110 zipo katika hatua mbalimbali za ujenzi, zikiwemo nyumba 50 za chini zilizofikia hatua ya mwisho na zinatarajiwa kuanza kutumika. Aidha, majengo mawili ya ghorofa tano yako katika hatua ya msingi, ambapo kila jengo litakuwa na uwezo wa kuhudumia familia 30.
Kwa mujibu wa Mndeme, TBA imeanza kushirikisha sekta binafsi katika utekelezaji wa mradi huo baada ya eneo hilo kutangazwa na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi kuwasilisha mapendekezo ya kushirikiana na Wakala.
Amesema mradi huo umepangwa kuwa na huduma muhimu zikiwemo shule za awali, shule mbili za msingi, maeneo ya biashara pamoja na vyuo.
Mndeme amesema mahitaji ya nyumba katika Jiji la Dodoma ni makubwa, akifichua kuwa wakati ujenzi wa nyumba 150 za awali ulipokuwa ukiendelea, TBA ilipokea zaidi ya maombi 1,000 kutoka kwa watumishi waliokuwa wakihitaji makazi.
Amesema hadi sasa, Meneja wa TBA Mkoa wa Dodoma ana maombi zaidi ya 8,000 ya nyumba kutoka kwa watumishi na wananchi, hali inayoonyesha ukubwa wa changamoto ya makazi katika jiji hilo.
Mndeme ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita na Wizara ya Ujenzi kwa kuendelea kuiwezesha TBA kupitia ruzuku, akisema mradi huo ulioanza mwaka 2021 umeendelea kutekelezwa kwa ufadhili wa Serikali.
Amesema TBA sasa inalenga kuongeza kasi ya ushirikishwaji wa sekta binafsi ili kuharakisha ukamilishaji wa mpango wa ujenzi wa nyumba 3,500 na hivyo kupunguza changamoto ya makazi katika Jiji la Dodoma.



Social Plugin